Obama, Cameron wamshinikiza Putin kuhusu Syria
14 Mei 2013Obama na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron walitaka kujenga hamasa mpya nyuma ya mkutano wa kimataifa wa Syria unaodhaminiwa na Marekani na Urusi, ambao sasa unatarajiwa kufanyika mwezi Juni, wakati wawili hao walipokutana mjini Washington.
Cameron, akiwa ndiyo amekamilisha ziara nchinin Urusi, alisema anaamini London, Washington na Moscow wamepata muafaka juu ya mgogoro wa Syria, ambao umegharimu maisha ya maelfu ya watu. Obama alisema Urusi ina maslahi na wajibu wa kusaidia kukomesha mgogoro huo, akisema alikuwa amewasilisha ujumbe kwa rais Vladmir Putin kabla ya ziara ya waziri wake wa mambo ya kigeni mjini Moscow wiki iliyopita.
Hali bado ni ngumu sana Syria
Lakini, Obama alionya kuwa itakuwa vigumu sana kuishawishi Urusi kubadilisha msimamo wake, na kubainisha kuwa bado kuna tofauti za msingi kati ya nchi hiyo na mataifa ya magharibi. Obama alisema hata kama Urusi itashawishika na kusimama upande wao, hali nchini Syria bado ni ngumu sana kutokana na ushiriki wa Iran, kundi la Hezbollah na wapiganaji walio na mafungamano na mtandao wa Al-qaeda katika mgogoro huo.
"Siahidi kuwa kutakuwepo na mafanikio. Ukweli ni kwamba miungu ya ghadhabu ikishaachiwa katika hali kama tunayoshuhudia nchini Syria, inakuwa vigumu sana kuweka tena mambo sawa," alisema Obama.
Cameron aonyesha matumaini
Kwa upande wake, waziri mkuu Cameron alikuwa mwenye matumaini zaidi, akisema anaamini London, Washington na Moscow zimefikia muafaka juu ya mgogoro huo. Cameron alisema kuwa historia ya Syria inaandikwa kwa kutumia damu ya raia wa nchi hiyo, huku dunia ikitizama tu, na kuongeza kuwa wakati umefika kwa dunia kuja pamoja na kukomesha umuagaji huu wa damu. Cameron pia aliahidi kuongeza msaada usio wa kijeshi kwa baadhi ya makundi ya waasi nchini Syria kwa mara mbili katika kipindi cha mwaka ujao.
"Kama hatuusaidii upinzani nchini Syria ambao tunautambua kuwa halali, na uliosaini tamko kuhusu mustakabali wa Syria yenye kidemokrasia, inayoheshimu haki za wachache, tusipofanya kazi na upande huo, basi tusishangae kuona makundi yenye itikadi kali yakizidi kuongezeka," alisema Cameron.
Hezbollah yaupiga tafu utawala wa Assad
Cameron na Obama walikutana huku kukiwa na ishara kuwa utawala wa Assad hautanguka kwa urahisi, wakati jeshi lake likipata mafanikio dhidi ya waasi katika mkoa muhimu wa Homs, kwa msaada wa kundi la Hezbollah, kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria.
Katika mkoa wa kusini wa Daraa, ambao ndiyo chimbuko la uasi dhidi ya Assad, jeshi la serikali lilichukua udhibiti wa mji wa Khirbet Ghazaleh, uliyoko katika njia kati ya Damascus na mpaka wa Jordan. Shirika hilo lilisema siku ya Jumatatu kuwa limeorodhesha vifo vya watu wapatao 82,257 tangu kuanza kwa vita hivyo Machi 2011, wakiwemo raia wa kawaida 34,473.
Katika ishara nyingine ya kuongezeka kwa juhudi za kidiplomasia, Ikulu ya kremlin imesema kuwa waziri mkuu wa Israel Benjanim Netanyahu atafanya mazungumzo na rais Putin leo, kujaribu kuishawishi nchi hiyo iachane na mpango wake wa kunedelea kuiuzia Syria silaha. Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon naye ataizuru Urusi siku ya Ijumaa, wakati waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akitarajiwa kuwa na mazungumzo na raias Obama mjini Washington leo.
Serikali, waasi bado kuthibitisha ushiriki wao
Mkutano wa Syria unaoandaliwa na Marekani na Urusi unatarajiwa kufanyika mwezi Juni, lakini taarifa za maandalizi yake bado hazijawekwa bayana. Wapinzani wamesema watashauriana na wafadhili wao - nchi za Saudi Arabia, Qatar na Uturuki kabla ya kuamua kushiriki katika mazungumzo hayo, huku Syria nayo ikisema inataka ipewe maelezi kamili juu ya mkutano huo kabla ya kuamua kuhusu ushiriki wake.
Waziri wa mawasiliano Omran Zoabi, amesema Syria inakaribisha pendekezo hilo, lakini akasisitiza kuwa nchi yake haitakuwa sehemu ya mkutano unaoumiza uhuru wa Syria kwa njia yoyote ile. Zoabi aliongeza kuwa uamuzi juu ya jukumu la rais Bashar al-Assad uko mikononi mwa raia wa Syria tu kupitia sanduku la kupigia kura.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman.