Jeshi la Syria ladhibiti barabara muhimu sasa
13 Mei 2013Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameishutumu Syria kwa kujaribu kuiingiza nchi yake katika mzozo wa Syria baada ya mashambulio mawili ya mabomu yaliyoua watu 46 katika mji wa mpakani
Waasi wanaopigana kuuondoa utawala wa rais Bashar al-Assad nchini Syria wanajaribu kupambana kutokea katika eneo la karibu ya mpaka na Jordan na kuingia upande wa jimbo la kusini la Daraa, katika kile kinachoonekana kama njia muafaka ya kuweza kuukamata mji mkuu Damascus.
Waasi wapata pigo
Wiki chache zilizopita , waasi walipata mafanikio makubwa , lakini hivi karibuni wamepata pigo kutokana na mashambulio ya jeshi la serikali.
Majeshi ya serikali yameukamata mji wa Khirbet Ghazaleh siku ya Jumapili na waasi walikimbia kutoka eneo hilo, amesema Rami Abdul-Rahman, mkuu wa shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza.
Majeshi ya serikali yalifungua tena barabara hiyo , na kurejesha uwezo wa barabara hiyo kupeleka vifaa baina ya Damascus na mji mkuu wa jimbo la Daraa ambao unaowaniwa na jeshi hilo.
Waasi wanadhibiti sehemu kubwa ya ndani ya nchi hasa upande wa kaskazini wa Syria , lakini maeneo hayo yako mbali kutoka mji mkuu kuliko mpaka na Jordan.
Pendekezo la Urusi na Marekani kujadiliwa
Kundi kuu la upinzani nchini Syria la muungano wa kitaifa litakutana Mei 23 kujadili pendekezo la Urusi na Marekani la kufanyika mkutano wa kimataifa kuhusu suluhisho la kisiasa katika mzozo wa nchi hiyo.
Msemaji wa muungano huo Sonir Ahmed ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mkutano huo utafanyika mjini Istanbul nchini Uturuki .
Pendekezo la Marekani na Urusi lililotangazwa mjini Moscow wiki iliyopita, linatoa wito wa kufanyika mkutano wa kimataifa kuyapa nguvu makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana mjini Geneva kwa ajili ya suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Syria.
Makubaliano ya Geneva yanatoa wito wa kusitishwa kwa matumizi ya nguvu na kuundwa kwa serikali ya mpito.
Waziri mkuu aonya
Wakati huo huo waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema jana kuwa Uturuki imewakamata watu tisa kuhusiana na mashambulio mawili ya mabomu yaliyotegwa katika gari ambayo yamesababisha vifo katika mji wa Reyhanli, lakini serikali ya Syria imekana kuhusika na shambulio hilo.
Tunapaswa kuwa watulivu zaidi. Uchokozi huu una lengo lake, ambao ni kuiingiza Uturuki katika vita vya Syria.
Serikali ya Uturuki imesema kuwa inawashikilia watuhumiwa wawili ambao wamekiri na kuishutumu Syria kwa kujaribu kuiingiza Uturuki katika mzozo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Mashambulio hayo ni tukio baya kabisa katika kile ambacho wachunguzi wanaona kuwa ni kuendelea kutumbukia nchi za eneo hilo katika mzozo wa Syria ambao ulianza Machi mwaka 2011.
Akizungumza wakati wa ziara yake mjini Berlin waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Ahmet Davutoglu ameyaita mashambulio hayo kuwa ni ukiukaji wa mstari wa Uturuki, na kuonya kuwa nchi yake inahaki ya kuchukua hatua yoyote inayostahili.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe
Mhariri:Yusuf Saumu