1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awasili Senegal

Admin.WagnerD27 Juni 2013

Rais wa Marekani Barrack Obama atatoa heshima zake za kutambua mateso ya utumwa na ukomavu wa kidemokrasia nchini Senegal licha ya kuwa katika eneo linalokumbwa na misukosuko katika ziara yake ya pili barani Afrika.

https://p.dw.com/p/18xKb
Picha: Reuters

Rais Obama aliwasili katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, jana usiku anakoanzia ziara ya nchi tatu za Afrika ikiwemo Afrika kusini na Tanzania katika jitihada za utawala wake kuyatimiza matarajio ya bara hilo ambalo ndilo chimbuko la asili yake.

Anaandamana na mkewe Michelle Obama na binti zake wawili Sasha na Malia na ziara yake hiyo imegubikwa kwa kiasi fulani na hali ya afya ya shujaa wa Afrika Nelson Mandela ambayo inazidi kuzorota akiwa amelazwa katika hospitali mjini Pretoria na kutishia kuvuruga ratiba ya Obama nchini Afrika ya Kusini.

Rais wa Marekani Barrack Obama alipowasili Senegal
Rais wa Marekani Barrack Obama alipowasili SenegalPicha: Reuters

Rais huyo wa Marekani leo anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Macky Sall ambapo watazungumzia umuhimu wa uzingativu wa sheria katika mahakama ya juu nchini humo. Baada ya mazungumzo hayo atafanya mkutano na waandishi wa habari.

Baadaye leo Obama na familia yake watatembea kisiwa cha Goree ambacho ni kumbukumbu ya yaliyokuwa maeneo ya biashara za watumwa ambayo pia yametembelewa na marais wa zamani wa Marekani, George W Bush na Bill Clinton.

Demokrasia nchini Senegal inasifika

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Senegal, Fernand Tona, amesema kuwa ziara hii ya Obama inaashiria kile alichokiita kutuzwa medali ya dhahabu kwa nchi hiyo kutokana na kutambua kuweko kwa demokrasia katika taifa hilo lenye waislamu wengi lenye idadi ya wakazi milioni 13 na kuwa nchi pekee magharibi mwa Afrika ambayo haijashuhudia mapinduzi ya serikali.

Tona hata hivyo amesema kuwa ziara hii isitarajiwe kuimarisha uchumi wa taifa hilo kwani kuna mageuzi mengi ambayo bado yanahitaji kutekelezwa ili kuwavutia wawekezaji kutoka Marekani.

Hali ya Mali kujadiliwa

Inatarajiwa pia Rais Obama ataizungumzia hali ya nchi jirani na Senegal, Mali, kabla ya kikosi cha Umoja wa Mataifa kuanza operesheni zao nchini humo kukabiliana na makundi ya kiislamu yenye itikadi kali.

Rais Obama na mtoto wa kiafrika
Rais Obama na mtoto wa kiafrikaPicha: picture-alliance/dpa

Baada ya ziara yake nchini Senegal, Obama ataelekea Afrika kusini ambako alitarajiwa kukutana na Rais wa zamani, Nelson Mandela, lakini kutokana na hali yake haitawezekana. Hata hivyo viongozi hao wawili walikutana mwaka 2005 mjini Washington, Marekani wakati Obama alipokuwa amechaguliwa Seneta na wameshazungumza mara kadhaa kwa njia ya simu.

Ziara yake inapaswa kuangazia ukuaji wa kiuchumi wa bara hilo na nafasi zinazojitokeza katika nyanja hiyo pamoja na masuala ya vijana na afya na kutilia mkazo ushirikiano wa Marekani katika bara la Afrika ambalo linanufaika na wimbi la uwekezaji wa China.

Hata hivyo kumekuwa na hali ya kuvunjika moyo barani humo baada ya kuchaguliwa kwa Rais huyo wa Marekani mwenye asili ya Afrika mwaka 2008 na kuzua hisia za matumaini ya kuwa atazipa kipaumbele sera kuhusu Afrika katika ajenda ya uongozi wake lakini hilo bado halijaafikiwa kama ilivyotarajiwa na wengi kutoka barani humo.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/afp
Mhariri: Josephat Charo