1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela aifunika ziara ya Obama

26 Juni 2013

Rais Barack Obama anaanza ziara iliyosubiriwa kwa hamu barani Afrika, huku hali ya Nelson Mandela ikionekana kuiziba ziara hiyo, kwani macho na masikio yote yameelekezwa Afrika ya Kusini ambako Mandela yu mahututi.

https://p.dw.com/p/18wzN
U.S. President Barack Obama wipes his forehead as he speaks about his vision to reduce carbon pollution while preparing the country for the impacts of climate change while at Georgetown University in Washington, June 25, 2013. REUTERS/Larry Downing (UNITED STATES - Tags: POLITICS ENVIRONMENT) / Eingestellt von wa
USA / Barack Obama / Schweiß / Rede zum KlimaschutzPicha: Reuters

Familia ya Rais Obama inaondoka leo (26.06.2013) kwa ziara ya wiki moja barani Afrika itakayoifikisha nchini Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania kwa kile ambacho Ikulu ya Marekani inasema ni kuhamasisha demokrasia na fursa za kiuchumi kwenye bara hilo lililo asili ya wazazi wa familia hiyo.

Lakini hali inayozidi kuzorota ya afya ya Mandela inaonekana kuitanda ziara ya Obama.

Shaka kwamba kiongozi huyo ambaye ni alama ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani anaweza kuiaga dunia ndani ya siku chache zijazo, imezusha wasiwasi juu ya ratiba ya Rais Obama.

Tayari Ikulu ya Marekani imesema kwamba itashauriana na familia ya kiongozi huyo wa ukombozi nchini Afrika ya Kusini kuona ikiwa familia ya Obama inaweza kumtembelea hospitalini.

Mandela ni shujaa wa Obama

Binafsi, Obama amewahi kumtaja Mandela mara kadhaa kama shujaa wake wa kisiasa, lakini tayari Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika ya Kusini, Maite Nkoane Mashebane, ameshasema kwamba ombi hilo halitawezekana kutekelezwa kwa kuwa Mandela yuko kwenye hali mbaya.

Mzee Nelson Mandela katika sherehe yake ya kuzaliwa miaka minne iliyopita.
Mzee Nelson Mandela katika sherehe yake ya kuzaliwa miaka minne iliyopita.Picha: picture-alliance/dpa

Mara ya mwisho Obama kuonana na Mandela ilikuwa ni mwaka 2005, pale Mandela alipokuwa mjini Washington, Marekani, na Obama akiwa ndio kwanza amechaguliwa kuwa seneta.

Hata hivyo, viongozi hao wawili wamewahi kuzungumza kwa njia ya simu mara kadhaa baada ya hapo, ingawa hapajawahi kuwapo kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya maraisi hao wawili wa kwanza weusi kwa mataifa yao, tangu Obama kuingia madarakani mwaka 2008.

Ikulu ya Marekani inaichukulia ziara hii ya Obama kama nafasi ya kufidia muda mrefu ambao Rais Obama ameshindwa kupanga safari ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mara ya mwisho Obama kutembelea sehemu hiyo ya Afrika, ilikuwa ni pale aliposimama kwa muda nchini Ghana, mwaka 2009.

Fadhaa za Waafrika dhidi ya Obama

Tangu mwanzo baadhi ya wachambuzi waliichukulia ziara hii ya Obama kama yenye lengo la kupunguza fadhaa za Waafrika kwa kiongozi huyo wa taifa kubwa duniani na mwenye asili ya bara hilo, lakini aliyeonekana kulipuuzia kwenye awamu ya kwanza ya uraisi wake.

Wakati Nelson Mandela alipotoka jela mwaka 1990.
Wakati Nelson Mandela alipotoka jela mwaka 1990.Picha: picture-alliance/dpa

Tayari ratiba ya Obama barani Afrika imeitenga Kenya na kuwakera wengi nchini humo, nchi ambayo ni nyumbani kwa baba mzazi wa Obama na ambako ndiko pia waliko ndugu zake wake wa ubabani.

Na sasa, ikiwa afya ya Mandela ndiyo itakayoamua jaala ya ziara ya Obama barani Afrika, na kwa hivyo kutokea uwezekano wa kushindwa kuzitembelea baadhi ya sehemu, kwa kushindwa kurefusha ratiba yake, hilo litaongeza fadhaa zaidi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Josephat Charo