1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atangaza "njia sifuri" Afghanistan

26 Februari 2014

Rais wa Marekani Barack Obama amemuambia Hamid Karzai wa Afghanistan kuwa ataondoa wanajeshi wake wote nchini humo, kutokana na kushindwa kwa Karzai kusaini makubaliano ya pamoja ya ulinzi.

https://p.dw.com/p/1BFQn
Karzai und Obama
Picha: picture-alliance/dpa

Obama aliliacha suala la kuzungumzua na rais Karzai kwa wafanyakazi wake, lakini baada ya miezi tisa ya ukimya, alimpigia na kumuambia kuwa ingawa Marekani inataka kuendelea kuwepo nchini Afghanistan, wamepoteza matumaini kwamba Karzai angesaini makubaliano ya ulinzi, ambayo yangewapa ulinzi wa kisheria wanajeshi na makandarasi wa Marekani.

Kwa hiyo zaidi ya miaka 12 tangu uvamizi, Marekani imeanza kupanga kile inachokiita njia ya 'sifuri' - ambayo ni kuondoa wanajeshi wake wote, huku ikionya kuwa kutakuwa na madhara kadiri anavyozidi kuchelewa.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel alipowatebelea wanajeshi wa Marekani mjini Kabul
Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel alipowatebelea wanajeshi wa Marekani mjini KabulPicha: Reuters

"Kadiri tunavyozidi kwenda bila kusaini makubaliano ya BSA, Operesheni yoyote inayopangwa baada ya 2014 itakuwa ndogo kiviwango na kimalengo kwa sababu ya mahitaji ya mipangilio ya uwepo wa vikosi hivyo," alisema Jay Carney ni msemaji wa ikulu ya White House.

NATO kuijadili njia ya 'sifuri'

Obama alimuambia Karzai kuwa ameiagiza wizara ya ulinzi kuhakikisha kuwa ina mipango ya kutosheleza kukamilisha uondoaji uliopangiliwa vizuri kufikia mwishoni mwa mwaka. Marekani inataka kubakiza hadi wanajeshi 10,000 nchini humo ili watoe mafunzo na ushauri kwa vikosi vya taifa vya usalama vya Afghanistan, na pia kuendelea kuwasaka masalia wa Al-Qaeda.

Chuck Hagel, waziri wa ulinzi wa Marekani alisema mipango kwa ajili ya njia ya Sifuri ilikuwa hatua ya busara kwa kuzingatia kuwa rais Karzai ameonyesha wazi kuwa hana mpango wa kutia saini makubaliano hayo. Hagel aliondoka kwenda mjini Brussels kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa mataifa yanayounda Jumuiya ya kujihami ya NATO, na alisema atajadiliana na mawaziri hao kuhusu mipango hiyo mipya.

Marekani ina wanajeshi wapatao 33,600 nchini Afghanistan hivi sasa, na inawaondoa wanajeshi hao katika kutekeleza azma ya Obama ya kuhitimisha operesheni hiyo ya miaka 12 ambayo ilianza baada ya mashambulizi ya Spetemba 11 mwaka 2001.

Raia wa Afghanistan akiwapita wanajeshi wa Marekani walioko katika operesheni ya ulinzi.
Raia wa Afghanistan akiwapita wanajeshi wa Marekani walioko katika operesheni ya ulinzi.Picha: picture alliance / AP Photo

Masharti ya rais Karzai

Obama alizungumza na Karzai kwa mara ya mwisho Juni 25 mwaka jana kwa mujibu wa taarifa za ikulu ya White House. Karzai anasisitiza kuwa Marekani lazima isitishe operesheni na mashambulizi ya angani dhidi ya vijiji vya Aghanistan na maeneo ya makaazi, ianzishe mazungumzo ya amani na kundi la Taliban, na kuwaachia wafungwa wa Taliban kutoka gereza la Guantanamo nchini Cuba, kabla hajasaini makubaliano hayo.

Mwezi huu Afghanistan iliwaachia wapiganaji 65 wa Taliban kutoka gereza la Bagram, na kupuuza upinzani wa maafisa wa kijeshi wa Marekani waliosema kuwa wafungwa hao walikuwa hatari na kwamba wangerejea katika uwanja wa vita kuyashambulia majeshi ya NATO na Afghanistan.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,rtre,afpe
Mhariri: Josephat Nyiro Charo