1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan yawaachia wafungwa, Marekani yakasirika

13 Februari 2014

Afghanistan imewaachia kutoka jela wafungwa 65 ambao wanashukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Taliban, ambao Marekani inawatuhumu kuuwa wanajeshi wa NATO na wa Afghanistan pamoja na raia.

https://p.dw.com/p/1B7qz
Wafungwa wakiachiwa kutoka gereza la Bagram
Wafungwa wakiachiwa kutoka gereza la BagramPicha: picture-alliance/dpa

Wafungwa hao walifunguliwa milango ya gereza la Bagram asubuhi ya leo na kuruhusiwa kuondoka. Hayo yamethibitishwa na Abdul Shukor Dadras, mjumbe wa kamati ya serikali ya uchunguzi. Dadras amesema kesi za wafungwa hao zilikuwa zimechunguzwa vya kutosha, na hawakuona sababu yoyote ya kuendelea kuwazuia.

Kamanda wa jeshi la polisi ambalo linahusika na usalama wa gereza la Bagram, Luteni Jenerali Ghulam Farouq, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa baada ya kutoka gerezani, wafungwa hao ambao sasa ni raia huru walipanda magari na kuelekea nyumbani kwao. ''Sisi tumewaachia kutoka gerezani, hatuhusiki na namna wanavyoondoka, hatukuwapa usafiri,'' alisema kamanda huyo.

Marekani yaelezea kukerwa kwake

Mara tu baada ya kuachiwa wafungwa hao, ubalozi wa Marekani nchini Afghanistan umetoa tangazo kali, ukisema hatua hiyo ni ya kusikitisha, na inaweza kuchochea ghasia zaidi nchini Afghanistan. ''Serikali ya Afghanistan itawajibika kwa matokeo ya uamuzi wake, tunaitolea wito serikali hiyo kufanya kila iwezalo, kuhakikisha kuwa wale walioachiwa hawafanyi vitendo vingine vya kihalifu na vya kigaidi''. Lilisema tangazo hilo.

Marekani inawatuhumu wafungwa katika gereza hili la Bagram kuwa wahalifu sugu
Marekani inawatuhumu wafungwa katika gereza hili la Bagram kuwa wahalifu suguPicha: MASSOUD HOSSAINI/AFP/Getty Images

Kabla ya wafungwa hao kuachiwa, Jeshi la Marekani lilikuwa limetoa tamko, likisema walihusika moja kwa moja kuwauwa wanajeshi 32 wa Marekani na washirika wake wa NATO, pamoja na Waafghanistan 23, mchanganyiko wa wanajeshi na maafisa wa usalama na raia.

Katika tamko hilo jeshi la Marekani lilitaja majina na maelezo kamili ya watatu miongoni mwa hao walioachiwa, akiwemo Mohammed Wali, ambaye limemuita mtaalamu wa kundi la Taliban wa kuunda mabomu, ambayo yalitumiwa kuwashambulia wanajeshi katika jimbo la Helmand.

Karzai haambiwi chochote

Lakini rais wa Afghanistan Hamid Karzai amesema gereza hilo la Bagram ambalo liko umbali wa kilometa 50 kaskazini mwa mji mkuu, Kabul, limekuwa likisaidia kampeni ya kundi la Taliban, akidai baadhi ya wafungwa waliteswa hadi kuichukia nchi yao. Gereza hilo lilikuwa likichungwa na jeshi la Marekani hadi lilipokabidhiwa kwa serikali ya Afghanistan mwaka uliopita.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan anaamini udhibiti wa gereza la Bagram ni muhimu kwa uhuru wa nchi yake
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan anaamini udhibiti wa gereza la Bagram ni muhimu kwa uhuru wa nchi yakePicha: Johannes Eisele/AFP/Getty Images

Majariwa ya wafungwa wanaosalia katika gereza hilo imekuwa homa ya muda mrefu ya rais Karzai, ambaye analichukulia gereza hilo kama alama ya nchi yake kurejeshewa uhuru wa kujiamulia mambo.

Baadhi ya wachambuzi wanasema serikali ya Afghanistan inaamini kwamba kuwaachia wafungwa hao kutaupa msukumo mchakato wa mazungumzo yaliyokwama kati yake na kundi la Taliban. Karzai amekwenda nchini Uturuki leo, ambako atakutana na waziri mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif, na inaaminika suala la kuanzisha mazungumzo na Taliban litakuwa kwenye ajenda ya mkutano wa viongozi hao.

Uamuzi wa kuwaachia wafungwa hao unatarajiwa kuzidisha uchungu katika mahusiano baina ya Afghanistan na Marekani na washirika wake, ambao wanafanya maandalizi ya kuondoa vikosi vyao nchini humo, baada ya kuwepo kwa miaka 13.

Rais wa Afghanistan alifanya uamuzi wa kushtukiza mwaka jana pale alipokataa kutia saini mkataba wa usalama kati yake na Marekani, ambao ungeruhusu wanajeshi 10,000 wa kimarekani kubaki nchini Afghanistan baada ya wenzao kuondoka mwishoni mwa mwaka huu. Hata hivyo, mazungumzo kuhusu mkataba huo bado yanaendelea..

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo