1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aung San Suu Kyi anusa madaraka

12 Novemba 2015

Rais wa Marekani Barack Obama amempongeza rais wa Myanmar Thein Sein kwa uchaguzi wa kihistoria, uliokipa ushindi chama cha Aung San Suu Kyi. Katika kura zilizohesabiwa chama hicho kimepata asilimia 85.

https://p.dw.com/p/1H4NE
Wananchi wa Myanmar wakishangilia ushindi wa chama cha Upinzani
Wananchi wa Myanmar wakishangilia ushindi wa chama cha UpinzaniPicha: Reuters/J. Silva

Msemaji wa Serikali ya Myanmar ambaye pia ni waziri wa habari wa nchi hiyo Ye Htut ambaye ametangaza pongezi za rais Obama, amesema rais huyo wa Marekani amesifu jinsi uchaguzi wa Jumapili nchini ulivyokuwa huru na wa kuaminika.

Ikiwa matokeo kamili ya uchaguzi huo yataendelea katika mkondo wa yale yaliyokwishatangazwa, Suu Kyi na chama chake cha National League for Demokracy, NDL ataupiga kumbo utawala wa majenerali wa kijeshi walioitawala nchi hiyo hadi rais wa sasa Thein Sein alipoanzisha mabadiliko makubwa ya kidemokrasia miaka minne iliyopita.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Myanmar, rais Obama ameahidi kuendeleza ushirikiano na serikali ya nchi hiyo.

Mafanikio ya sera za nje za Obama

Rais Obama aliizuru Myanmar mara mbili katika kipindi cha miaka 3 iliyopita, akiwa na matumaini kwamba mabadiliko ya kidemokrasia katika taifa hilo yatakuwa mafaniko ya kidiplomasia katika utawala wake.

Rais Barack Obama ameizuru mara mbili Myanmar katika muda wa miaka mitatu
Rais Barack Obama ameizuru mara mbili Myanmar katika muda wa miaka mitatuPicha: Reuters/K. Lamarque

Tayari rais Thein Sein na Mkuu wa jeshi la Myanmar Min Aung Hlaing wameutambua ushindi wa Suu Kyi, na wamempongeza kwa ushindi wake katika uchaguzi huo wa kwanza huru kuwahi kuitishwa baada ya kupita miaka 25.

Viongozi hao wawili hali kadhalika wameelezea utayarifu wao wa kuheshimu matokeo, na kukubali pendekezo la Aung San Suu Kyi kufanyika mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa, lakini bado vyama havijakubaliana juu ya mada ya mazungumzo hayo.

Bado wamyanmar hawajaamini

Hata hivyo, mashaka yanabakia miongoni mwa wananchi wa Myanmar, kama mara hii wanajeshi watakubali kukabidhi madaraka kwa mshindi, kama anavyoeleza mmoja wao, Maung Shwe:

''Nina mashaka kidogo kuhusu kukabidhi madaraka, kwa sababu hali kama hii ilishatokea hapa katika uchaguzi wa 1990'' amesema Shwe na kuongeza kuwa bado kumbukumbu hiyo wanayo na haitaondoka katika mawazo yao.

Tangazo la serikali limejaribu kuyaondoa mashaka hayo, likisema itayaheshimu maamuzi ya raia, na itakabidhi madaraka kwa muda uliowekwa. Hali kadhalika, tangazo hilo limeuhakikishia umma kwamba rais wa nchi hiyo atashirikiana na watu wengine katika kuhakikisha usalama na utengamano wa nchi baada ya uchaguzi huu.

Rais wa Myanmar Thei Sein ambaye anapongezwa kwa kusimamia mageuzi ya kidiplomasia
Rais wa Myanmar Thei Sein ambaye anapongezwa kwa kusimamia mageuzi ya kidiplomasiaPicha: Reuters/Soe Zeya Tun

Lakini jeshi nchini Myanmar linaendela kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za nchi hiyo, limetengewa asilimia 25 ya viti vyote bungeni kwa mujibu wa katiba. Juu ya hayo kamanda mkuu wa jeshi hilo anaachiwa uwezo wa kuwateuwa mawaziri muhimu watatu, wakiwemo wa ulinzi, mambo ya ndani na ilinzi wa mipaka ya nchi.

Udhibiti wa wizara ya ndani unalipa jeshi uwezo wa kusimamia shughuli za utawala wa ndani, hali ambayo ni changamoto kwa Aung San Suu Kyi katika kutekeleza sera za chama chake. Bado Suu Kyi hajatoa maelezo kuhusu namna atakavyoishughulikia changamoto hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe

Mhariri:Hamidou Oummilkheir