1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suu Kyi atoa wito wa kufanyika mazungumzo ya maridhiano

11 Novemba 2015

Aung San Suu Kyi ameomba kufanya mazungumzo aliyoyataja ya 'maridhiano ya kitaifa' kati yake, Rais na mkuu wa majeshi Myanmar huku chama chake cha NLD kikitarajiwa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/1H3qs
Picha: Getty Images/AFP/N. Asfouri

Chama hicho cha NLD kinachounga mkono misingi ya demokrasia Myanmar kinasubiri kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Jumapili iliyopita baada ya kujinyakulia asilimia tisini ya viti vilivyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo.

Licha ya kuwa maafisa wa tume hiyo ya uchaguzi hawajakitangaza rasmi chama hicho cha Aung Suu Kyi mshindi, sura ya kisiasa nchini Myanmar ambayo imekuwa ikitawaliwa na jeshi na washirika wake kwa miongo mingi inaonekana itachukua sura mpya.

NLD yasubiri matokeo kwa hamu

Wafuasi wa Suu Kyi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel wanasubiri kwa hamu na ghamu kuona hali hiyo ya kisiasa itakuwaje na jeshi litapokea vipi ushindi wa NLD huku bado kumbukumbu ya hali ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 1990 ambapo NLD ilishinda lakini jeshi likasalia kuwa na udhibiti mkubwa katika uongozi ikiwa bado akilini mwa wafuasi hao wa NLD.

Wafuasi wa NLD wakiwa wamekusanyika nje ya makao makuu ya chama chao
Wafuasi wa NLD wakiwa wamekusanyika nje ya makao makuu ya chama chaoPicha: Reuters/J. Silva

Suu Kyi amemuandikia Rais Thein Sein, mkuu wa majeshi Min Aung Hlaing na spika wa bunge Shwe Mann barua inayosema wananchi wameelezea ari na nia zao katika uchaguzi na hivyo anawaalika kwa mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa kwa wakati wanaoridhia.

Waziri wa habari wa Myanmar Hy Htut amesema Sein amekubali kuhudhuria mkutano huo punde matokeo rasmi ya uchaguzi yatakapotangazwa.

Hatua ya Suu Kyi kuridhia kufanya mazungumzo na viongozi ambao wamemuweka katika kifungo cha nyumbani kwa miaka 15 kunaonyesha kujitolea kwake kushirikiana na mahasimu wake na kuitanzua nchi hiyo kutoka siasa za kiimla.

Wachambuzi wanasema kutakuwa na kipindi cha miezi kadhaa migumu kisiasa nchini Myanmar huku katiba iliyoandikwa na jeshi ikilipa jeshi asilimia 25 ya viti bungeni na nyadhifa kuu katika sekta ya usalama na ulinzi.

Je jeshi litasalia kuwa na ushawishi kwa kiasi gani?

Katiba hiyo pia inamzuia Suu Kyi mwenye umri wa miaka 70 kuwa rais wa nchi hiyo licha ya ushawishi wake mkubwa katika kuleta demokrasia nchini humo na kuikwamua nchi hiyo kutoka kutengwa kwa muda mrefu na Jumuiya ya kimataifa. Mshindi huyo wa tuzo ya amani Nobel amesema bila shaka atakuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ijayo.

Spika wa bunge Shwe Man na Rais Thein Sein
Spika wa bunge Shwe Man na Rais Thein SeinPicha: Reuters/Soe Zeya Tun

Hii leo maafisa wa tume ya uchaguzi wamesema chama cha NLD kimeshinda viti 163 kati ya viti 182 vya mabunge yote vilivyotangazwa kufikia sasa na matokeo rasmi yanatarajiwa katika kipindi cha siku kumi zijazo. Suu Kyi ameshinda tena kiti chake cha jimbo la Kawhmu.

NLD inahitaji asilimia 67 kuwa na wingi wa viti bungeni na kukiwezesha kuunda serikali ijayo na kuwa na usemi zaidi katika bunge jipya. Spika wa bunge Shwe Mann jenerali wa zamani wa jeshi ambaye alishindwa katika jimbo lake anatajwa kuwa huenda akawa rais licha ya kuwa umaarufu wake ndani ya chama tawala cha Union Solidarity and Development USDP umepungua.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman