1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yashambuliwa kwa kumpokea al-Bashir

16 Julai 2013

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Nigeria wamefikisha kesi katika mahakama kuu mjini Abuja, wakiitaka kutoa waranti wa kumkamata rais wa Sudan Omar al-Bashir aliyekwenda huko kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika.

https://p.dw.com/p/198GX
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan na rais wa Sudan Omar al-Bashir mjini Abuja
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan na rais wa Sudan Omar al-Bashir mjini AbujaPicha: DW/U. Musa

Wanaharakati hao wa kutetea haki za binadamu ambao walikasirishwa na hatua ya Nigeria kumkaribisha Omar al-Bashir ambaye anatuhumiwa kupanga mauaji ya kimbari na uhalifu mwingine wa kivita, waliitaka mahakama ya kimataifa iifikishe Nigeria mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kwa kushindwa kumkamata rais huyo wa Sudan na kumpeleka katika mahakama ya ICC nchini Uholanzi.

Shirika la kutetea haki za kiuchumi na kijamii pamoja na uwajibikaji nchini Nigeria, limetoa rai kwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan kuunga mkono matakwa ya jumuiya ya kimataifa kuwatendea haki wahanga wa mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita.

Rais al-Bashir anatafutwa na ICC kwa tuhuma za uhalifu wa kivita jimboni Darfur
Rais al-Bashir anatafutwa na ICC kwa tuhuma za uhalifu wa kivita jimboni DarfurPicha: picture-alliance / dpa

Mwaliko wa Umoja wa Afrika

Lakini naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Nigeria Prof. Viola Onwuliri amesema Nigeria haina cha kufanya kwani haikutoa mwaliko kwa al-Bashir.

''Nigeria ni mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Afrika, na ni Umoja wa Afrika ambao unahusika kuamua nani anahudhuria. Kwa hivyo, ikiwa Umoja huo umeamua kumwalika rais yeyote, sisi hatuhusiki kwa vyovyote. Ni wajibu wa Umoja wa Afrika.'' Alisema Profesa Onwuliri.

Uingereza ambayo ni mkoloni wa zamani wa Nigeria, imetoa tamko linaloelezea kusikitishwa na hatua ya Nigeria kushindwa kumkamata al-Bashir. Waziri anayehusika na masuala ya Afrika Mark Simmonds amesema kushindwa huko kunakwamisha kazi ya ICC, na kutuma ujumbe mbaya kwa wahanga kwamba haki wanayoisubiri itacheleweshwa zaidi.

Al-Bashir aondoka mapema

Taarifa za hivi karibuni kutoka Abuja zinaeleza kuwa rais Al-Bashir ameondoka mjini humo kabla ya kumalizika kwa mkutano aliokwenda kuhudhuria. Mwanadiplomasia aliyetoa taarifa hiyo hata hivyo amekataa kusema iwapo kuondoka haraka kwa rais huyo kuna uhusiano na shinikizo la wanaharakati.

Nigeria Imesema Al-Bashir amealikwa na Umoja wa Afrika kama ilivyokuwa kwa marais wengine waliohudhuria mkutano.
Nigeria Imesema Al-Bashir amealikwa na Umoja wa Afrika kama ilivyokuwa kwa marais wengine waliohudhuria mkutano.Picha: DW/U. Musa

Jumapili, Omar al-Bashir alipokelewa kwa zuria jekundu nchini Nigeria. Alikuwa mmoja wa marais wanane waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika kuhusu ugonjwa wa Ukimwi. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pia alishiriki katika mkutano huo.

Baadhi ya nchi za kiafrika, zikiwemo Afrika Kusini, Malawi, Uganda, Kenya, Zambia na Jamhuri ya Afrika ya Kati zimetamka bayana kuwa Rais al-Bashir hakaribishwi kwenye ardhi zao, na kuonya kuwa akifanya hivyo atakamatwa.

Wanaharakati wameionya Nigeria, kwamba kwa kushindwa kumkamata rais Omar al-Bashir inaweza kuwekewa vikwazo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Lakini, nchi nyingine za kiafrika, zikiwemo Chad na Djibout ziliwahi kumkaribisha rais huyo wa Sudan na hazikuchukuliwa hatua yoyote.

Kuna maoni miongoni mwa waafrika wengi kwamba mahakama ya ICC iliyo na makao barani Ulaya, ina mwelekeo wa kibaguzi kwa kuwalenga waafrika peke yao.

Mwandishi:Daniel Gakuba/APE/RTRE

Mhariri: Ssessanga, Iddi Ismail