Al Bashir atishia kuizuwilia mafuta Juba
28 Mei 2013Mapigano hayo yaliripuka jumapili iliyopita katika eneo la Dandor,umbali wa kilomita 500 magharibi ya mji mkuu wa Sudan-Khartoum.
Msemaji wa jeshi la Sudan,kanali Sawarmy Khaled amesema vikosi vya serikali vimepigana na waasi walioushambulia mji wa Dondor na kuwauwa zaidi ya 70 pamoja na kuviteka vifaru vyao viwili.Taarifa ya kanali Khaled iliyotangazwa na kituo rasmi cha matangazo-.Radio Omdurman,haikusema hasara iliyopatikana upande wa vikosi vya serikali.
Hata hivyo,waasi kupitia msemaji wa jeshi la ukombozi wa watu wa kaskazini SPLA-N,Arnu Ngutullu Loddi amesema vikosi vya serikali vimepata hasara kubwa kutokana na mapigano hayo.
Hakuna habari huru zinazothibitisha madai ya upande wowote ule.
Wasai wameonya mapigano zaidi yataripuka dhidi ya vikosi vya serikali ya Sudan na wanamgambo wanaowaunga mkono.
Wengi kati ya wakaazi milioni moja na laki noja wa Kordofan Kusini wanasemekana kuelemea zaidi upande wa Sudan kusini na wanaishi katika eneo linalodhibitiwa na SPLA-N
Serikali ya mjini Khartoum kila kwa mara imekuwa ikiishutumu serikali ya Juba kuwaunga mkono waasi-madai yanayokanushwa kila wakati na Sudan kusini.
Al Basahir atishia kufunga mabomba ya mafuta
Rais Omar al Bashir wa Sudan ameonya atayafunga mabomba yanayoipatia mafuta Sudan kusini ikiwa Juba haitaacha kuwaunga mkono waasi.
Onyo hilo amelitoa katika hafla ya kusherehekea kukombolewa na jeshi la Sudan mji wa Abou Kershola toka mikononi mwa waasi wa Kordofan kusini.
"Tunaionya serikali ya kusini,wakiwapatia msaada wowote wapiganaji wa chama cha ukombozi wa Sudan -Kaskazini-SPLA-N,au waasi wa Darfur,tutayafunga mabomba yote" amesema rais al Bashir aliyehoji tunanukuu"tutapata habari wakiacha au wakiendelea kuwaunga mkono".Mwisho wa kumnukuu.
May sabaa iliyopita,serikali ya mjini Khartum ilisema mafuta ya kusini mwa Sudan yameanza kusafirishwa upya kupitia mabomba ya mafuta yaliyoko Heglig-mji wa Sudan ulioko karibu na mpaka na Sudan kusini.
Sudan Kusini imeanza kupatiwa mafuta baada ya kuzuwiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na kufuatia makubaliano kadhaa yaliyotiwa saini na nchi hizo mbili Machi mwaka huu,yakipanga ratiba maalum ya kuanza kupatiwa mafuta Sudan kusini.
Jimbo la Kordofan linakabiliwa na mapigano tangu takriban miaka miwili sasa -mapigano yaliyowasababisha malaki ya wakaazi kuyapa kisogo maskani yao na wengine kadhaa kuuwawa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/Reuters
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman