NEW YORK:UN yataka kufikiwa kwa maamuzi jinsi kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa
25 Septemba 2007Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema muafaka unatakiwa kufikiwa katika mazungumzo juu ya upunguzaji wa matumizi ya gesi zinazoathiri mazingira.
Ban Ki-moon alisema hayo katika mkutano wa siku moja uliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa jijini New York.
Akizungumza katika mkutano huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitaka kupunguzwa kwa matumizi ya gesi ya Carbon inayoathiri mazingira.
Amezitaka nchi zinazoendelea kuweka malengo ya kupunguza matumizi ya gesi hiyo na kubainisha jinsi ya kuyafikia.
Umoja wa Ulaya umeshakubaliana kupunguza utoaji wa gesi hiyo ya carbon kwa silimia 20 ifikapo mwaka 2020.Lakini Kansela wa Ujerumani amesema kuwa malengo hayo yanaweza kufikia asilimia 30 iwapo jumuiya nyingine za kimataifa zitafikia makubaliano kama hayo.
Gavana wa jimbo la Carlfonia nchini Marekani, Arnold Schwarzenegger ambaye ameanzisha sheria kali katika jimbo kupunguza matumizi ya nishati ya mafuta inayotoa gesi ya carbon alisema mataifa tajiri na masikini yote yana nafasi yake katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Viongozi kutoka nchi zaidi ya 80 wanaudhuria mkutano huo wakiwa ni miongoni mwa watu 150 wanaotarajiwa kuzungumza katika mkutano huo.
Mkutano huo uliyoitishwa na Umoja wa Mataifa unajaribu kuweka msingi kwa ajili ya mkutano mkubwa kabisa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa unaotarajiwa kufanyika katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia mwezi Decemba mwaka huu.