NEW YORK : Nyota wa muziki wapigia debe mazingira
8 Julai 2007Baadhi ya wanamuziki mashuhuri kabisa duniani kuanzia Red Hot Chili hadi Madonna na The Police wamepiga muziki moja kwa moja majukwaani hapo jana kuwahamasisha mashabiki na serikali kuchukuwa hatua kupambana na ongezeko la ujoto duniani.
Maelfu kwa maelfu ya watu walisherehekea muziki huo mjini Sydeny Australia,Tokyo Japani,Shanghai China,Hamburg hapa Ujerumani,Johannesburg Afrika Kusini,London Uingereza Washington na New Jersey Marekani pamoja na Rio de Janeiro nchini Brazil kwa kujiunga na wanamuziki Bon Jovi,James Blunt, Linkin Park,Shakira,Alicia Keys na wengine wengi.
Wakiongozwa na mwanaharakati wa mazingira makamo wa rais wa zamani wa Marekani Al Gore maonyesho hayo yalidumu kwa zaidi ya masaa 22.
Katika uwanja wa Giants ulioko nje ya mji wa New York Al Gore aliwashukuru watu wanaokadiriwa kufikia bilioni kutoka katika nchi zaidi ya 130 za mabara saba duniani waliosikiliza muziki huo moja kwa moja,kupitia TV au hata mtandao na kumtaka kila mtu kusaidia kutatuwa tatizo la hali ya hewa.