Netanyahu ziarani Marekani
4 Machi 2014Obama na Netanyahu si aina ya watu unaoweza kuwaita wameshibana. Uhusiano wao ni wa mashaka. Wanalumbana kwenye masuala kadhaa. Jim Phillips, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati katika Wakfu wa The Heritage mjini Washington, anasema viongozi hao wawili hao hawaivi chungu kimoja hata kama nchi zao zina uhusiano wa muda mrefu.
"Obama na Netanyahu wamegawika sio tu kwenye sera bali pia katika mitazamo yao ya kilimwengu na hata haiba zao. Hata hivyo, uhusiano kati ya Marekani na Israel umejengwa kwenye misingi imara, kiasi ya kwamba tafauti kati ya viongozi wawili wakuu haziwezi kuuvunja kabisa kabisa." Alisema Phillips.
Kwa Netanyahu, usalama wa Israel ndio kipaumbele cha pekee lakini katika siku za hivi karibuni Obama ameonesha kuwaelewa Wairan, wapinzani wakubwa wa Israel katika eneo hilo, hali ambayo imeukera sana utawala wa Netanyahu.
Disemba mwaka jana, Obama alisema kuwa hadhani ikiwa madai ya Israel kutaka kuharibiwa kabisa kwa vinu vya nyuklia vya Iran yanatekelezeka. Netanyahu amekuwa akishikilia kwamba makubaliano kati ya mataifa yenye nguvu duniani na Iran ni ya kupoteza muda na kwamba lazima Iran izuwiwe kwa namna yoyote kuwa na silaha za nyuklia.
Amani ya Mashariki ya Kati
Mchakato wa amani kati ya Israel na Palestina pia ni suala litakalochukuwa nafasi kubwa na ambalo linahitaji hatua za haraka zaidi. Wakati mazungumzo hayo ya amani yalipoanza tena mwezi Julai mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, aliweka muda wa mwisho kwa pande zote mbili kufikia makubaliano kuwa ni mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Kwa muda sasa kumekuwa na mkwamo na sababu ni uamuzi wa Israel kuendelea na mradi wake wenye utata wa kujenga makaazi ya walowezi kwenye ardhi za Wapalestina.
Kerry ameshakiri kwamba makubaliano ya amani hayaonekani kufikiwa, na sasa anapigania kupatikana angalau kwa mpango wa utaratibu wa mazungumzo, ambao ikiwa nao utakataliwa, "basi huenda ukazua matatizo makubwa kwa pande husika", anasema Natan Sachs wa Taasisi ya Brookings mjini Washington.
"Ikiwa Waisraili na Wapalestina wataukataa mpango wa Marekani, tunaweza kushuhudia mzozo hali ukiibuka, lakini ikiwa pande hizo mbili zitakubaliana japo kwa kiasi fulani, basi tutaona mabadiliko makubwa angalau kwenye siasa za ndani na nafasi ya kidiplomasia kwa pande zote mbili kusonga mbele." Aliongeza Sachs.
Inaaminika kuwa Obama atayatumia mazungumzo hayo ya leo kumtaka Netanyahu kusimamisha ujenzi wa makaazi ya walowezi, ingawa naye Netanyahu ameshasema mapema kwamba hatakubali shinikizo lolote kutoka kwa Obama.
Hata kama Obama naye, kama alivyo Kansela Angela Merkel, hakubaliani na kuiwekea vikwazo Israel kusitisha ujenzi huo, lakini kauli yake ni muhimu sana kwa wapinzani wa sera hiyo ya utanuzi wa makaazi ya walowezi.
Mwandishi: Gero Schließ
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo