Mabaraza ya mawaziri ya Ujerumani, Israel yakutana
25 Februari 2014Tayari mawaziri 14 kati ya 16 wa serikali kuu ya Ujerumani wako mjini Jerusalem kushiriki kwenye mkutano huo wa aina yake. Waziri wa Masuala Maalum, Peter Altmaier, hakupangiwa kuhudhuria mkutano huo, huku Makamu wa Kansela, Sigmar Gabriel, ambaye mwaka juzi alizusha hasira kali kutoka Israel pale alipoifananisha nchi hiyo na utawala wa ubaguzi wa rangi, alifuta safari yake dakika za mwisho kwa sababu ya kutojisikia vizuri, kwa mujibu wa msemaji wake.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani (dpa) serikali hizo mbili pia zinatarajiwa kusaini mikataba kadhaa, ikiwemo ule unaoziruhusu balozi za Ujerumani duniani kutoa huduma kwa wasafiri wa Israel katika nchi ambazo hazina uhusiano na dola hiyo ya Kiyahudi.
Kansela Angela Merkel ambaye aliwasili huko jana, alitumia fursa ya mazungumzo yake na viongozi wa Israel kutoa wito wa kukwamuliwa kwa mazungumzo kati ya Israel na Palestina, yanayosimamiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.
Muda wa mwisho uliowekwa kwa pande hizo mbili kupata rasimu ya makubaliano, ni tarehe 30 Aprili. Kuna wasiwasi kwamba endapo mazungumzo hayo yatafeli, basi Umoja wa Ulaya unaweza kuchukuwa hatua za kuiadhibu Israel.
Akiwa mjini Madrid kuelekea Tel Aviv, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, alikosoa vikali ujenzi huo wa makaazi ya walowezi kuwa sio tu ni jambo lisilosaidia, bali pia linaloharibu mchakato wa amani.
"Tunataka kuona kuna maendeleo hapa," alisema Kansela Merkel kabla ya mkutano wake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Jerusalem, akiongeza kwamba mgogoro huo wa Mashariki ya Kati lazima usulihishwe kwa kuwa na mataifa mawili huru, la Israel na la Palestina.
Merkel kutunukiwa nishani
Hiki ni kikao cha tano kufanyika katika kiwango cha mabaraza ya mawaziri, utaratibu ulioanza mwaka 2008, na baada ya kikao cha leo, Rais wa Israel Shimon Perez atamtunukia Kansela Merkel kile kinachoitwa Nishani ya Rais, ambayo ni heshima ya juu kabisa inayotolewa kwa taifa la Israel kwa watu ambao wametoa mchango mkubwa kwa taifa hilo au kwa ubinaadamu.
Israel inamtunukia Kansela Merkel nishani hiyo kwa kusimama pamoja na Israel na kwa mapambano yake dhidi ya hisia za chuki kwa Mayahudi na ukabila.
Ujerumani ni mshirika mkubwa wa Israel barani Ulaya, na Kansela Merkel anayetokea chama cha kihafidhina cha Christian Democrat, anaonekana kuwa na mapenzi makubwa kwa Israel.
Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, nchi za Ulaya, ikiwemo Ujerumani, zimekuwa zikiishutumu Israel kutokana na sera yake ya ujenzi wa makaazi ya walowezi.
Kote barani Ulaya kumekuwa kukitolewa wito wa kuigomea Israel kwa sababu ya ujenzi huo katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Jerusalem ya Mashariki. Hata hivyo, Netanyahu, alimsifu Merkel kama rafiki wa kweli kwa Israel, akisema mara kadhaa amepingana na hatua za kuigomea Israel.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman