Netanyahu azuru Marekani kuzuia mkataba na Iran
2 Machi 2015Ziara ya saa 48 ya waziri mkuu Netanyahu imezua ugomvi na rais wa Marekani Barack Obama na kuuvuruga uhusiano kati ya Marekani na Israel kufikia kiwango cha chini katika miaka iliyopita. Hotuba mbele ya wabunge wa Marekani hapo kesho itakayotolewa na kiongozi huyo wa Israel inalenga kutafuta uungwaji mkono wa dakika ya mwisho kuzuia uwezekano wa kuafikiwa makubaliano ya kimataifa na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Ziara ya Netanyahu imeikasirisha ikulu ya Marekani na wanasiasa mashuhuri wa chama cha Democratic kwa sababu hotuba ya kiongozi huyo bungeni ilipangwa na chama cha Republican bila kushauriana na rais, hatua inayokiuka itifaki. Wanasiasa kadhaa mashuhuri wa Marekani wanapanga kuisusia hotuba hiyo na hakuna mikutano yoyote iliyopangwa kati ya Netanyahu na maafisa wa serikali ya Marekani wakati wa ziara yake.
Muda mfupi kabla ndege yake kuondoka kutoka uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv, Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari anakwenda Washington akiwa na jukumu kubwa. "Naondoka kwenda Washington kwa kazi muhimu na ya kihistoria. Nahisi nawawakilisha wananchi wote wa Israel, hata wale ambao hawakubaliani na mimi, muwakilishi wa wayahudi wote. Nina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa Waisraeli na mustakabali wa taifa na watu wetu. Nitafanya kila kitu katika uwezo wangu kuulinda mustakabali wetu."
Netanyahu leo atalihutubia kundi la ushawishi la Marekani linaloiunga mkono Israel, AIPAC. Huku akitarajiwa kutangaza msimamo wake kuhusu Iran na kuwasilisha hoja nzito kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, kiongozi huyo anatarajiwa pia kutochochea hali ya wasiwasi iliyopo, ikizingatiwa kwamba Waisraeli wamechoshwa na kuingizwa katika mgogoro na mshirika wao mwenye nguvu kubwa duniani, Marekani.
Kandanda ya kisiasa
Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry, ambaye aliondoka Washington wakati Netanyahu alipokuwa akiwasili, amesisitiza kwamba Marekani inataka kuepusha siasa katika ziara ya Netanyahu yenye utata na hataki igeuzwe kuwa kandanda ya kisiasa.
Mshauri wa rais Obama wa masuala ya usalama wa kitaifa, Susan Rice, ameonya kwamba hotuba ya Netanyahu bungeni inahujumu uhusiano kati ya Marekani na Israel. Bi Rice aidha alisema mualiko uliotolewa na spika wa bunge John Boehner kwa Netanyahu wiki mbili kabla uchaguzi nchini Israel umesababisha mvutano kati ya chama cha Democratic na Republican ambao unavuruga msingi wa uhusiano kati ya Marekani na Israel.
"Sitataja malengo ya ziara ya waziri mkuu Netanyahu. Nadhani tumuache aseme mwenyewe. Lakini tunataka uhusiano kati ya Marekani na Israel uwe imara bila kutiliwa shaka wala kubadilika, bila kujali misimu ya kisiasa katika nchi zote mbili wala chama kipi kinachoongoza."
Bi Rice pia amesema, "Tumefanya kazi kubwa kufanikisha hilo na tutafanya kazi kwa bidii kuendeleza uhusiano huo."
Rais Obama amesema hatakutana na Netanyahu baada ya kulihutubia bunge kwa sababu ni karibu sana na uchaguzi wa Israel uliopangwa kufanyika tarehe 17 mwezi huu.
Makamu wa rais Joe Biden, ambaye kwa kawaida angetarajiwa kuwa mwenyekiti wa kikao muhimu kama hicho cha bunge, pia hatakuwepo kwa sababu amesema atakuwa na shughuli muhimu nje ya nchi zitakazomzuia kuhudhuria hotuba ya Netanyahu.
Mwandishi:Josephat Charo/AFPE/RTRE
Mhariri:Daniel Gakuba