Uhusiano wa Marekani na Israel mashakani
26 Februari 2015Washirika hao wawili Marekani na Israel wanaendelea kutupiana maneno wakati ikiwa imesalia siku sita tu kabla ya waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kutoa hotuba yake katika bunge la Marekani wiki ijayo, akiangazia vitisho vya nyuklia kutoka Iran.
Vuta nikuvute ilianza wakati Benjamin Netanyahu alipoyatuhumu mataifa yalio na nguvu duniani kwa kutelekeza ahadi ya kuizuwiya Iran kutengeneza silaha za nyuklia.
“Naiheshimu ikulu ya Marekani na rais wa Marekani Barrack Obama lakini ni jukumu langu kufanya kila niwezalo ili kuhakikisha usalama wa watu wa Israel” alisema Netanyahu kabla ya kuondoka kwenda Washington anakotarajiwa kutoa hotuba yake wiki ijayo siku ya Jumanne.
Lengo la Netanyahu ni moja tu kujaribu kuyasambaratisha mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yanayoongozwa na Marekani, hata kama hali hiyo inaweza kuhatarisha kuvunjika kwa mahusiano yake na Rais Obama. Waziri Mkuu huyo wa Israel anahofia mpango huo ambao upo katika hatua zake za mwisho za majadiliano unaweza kutoa nafasi kwa Iran kuomba kuwa na silaha za nyuklia baada ya muda wa kuizuwiya kufanya hivyo kukamilika.
John Kerry asema huenda Netanyahu akawa na maoni ambayo si sawa
Hata hivyo Waziri wa mambo ya nchi za nje wa MarekaniJohn Kerry ambaye amehusika katika mazungumzo ya kimataifa na Iran juu ya mpango wake wa nyuklia amesema Netanyahu huenda akawa amekosea.
"Sera yetu ni kwamba Iran haitopata silaha za nyuklia, Mtu yeyote anaekimbia huku na kule akisema kwamba hawapendi makubaliano, au hiki au kile, hajui makubaliano ni gani. Hakuna makubaliano yoyote kwa sasa na natoa tahadhari kwa watu kusubiri kuona majadiliano yatafikia wapi,” alisema John Kerry.
Kwa upande wake mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Susan Rice ameielezea hotuba ya Nentanyahu kama mkakati wa kuvunja mahusiano ya Marekani na Israel. Aidha rais Obama amekataa kuonana na Waziri Mkuu Netanyahu wakati wa ziara yake hiyo huku wademokrats wakiapa kutohudhuria hotuba hiyo. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Kerry pia hatokuwepo wakati wa ziara ya Netanyahu nchini humo.
Wachambuzi wanasema hii inatoa ishara kwamba Netanyahu si mgombea wanayempendelea katika uchaguzi wa Israel unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 mwezi ujao.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman