Ndege isiyokuwa na Rubani ya Marekani yadunguliwa Yemen
21 Agosti 2019Msemaji wa jeshi la waasi hao wa Houthi Yahya Saria awali alisema vikosi vyake vya jeshi la anga viliidungua ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani. Hata hivyo maafisa hao wa Marekani ambao hawakutaka majina yao kutajwa wameongeza kuwa ndege hiyo ilidunguliwa jana jioni.
Wamesema kwa sasa ni mapema mno kutambua moja kwa moja ni nani hasa aliyehusika na udunguaji wa ndege hiyo. Hii si mara ya kwanza kwa ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani kudunguliwa nchini Yemen.
Mwezi Juni mwaka huu jeshi la nchi hiyo lilisema waasi wa Houthi waliiangusha ndege ya aina hiyo kwa usaidizi wa Iran.
Vikosi vya Marekani mara kwa mara vimekuwa vikifanya mashambulizi ya angani kwa kutumia ndege hizo dhidi ya tawi la kundi la Al Qaida katika rasi ya kiarabu linalojulikana kama (AQAP).
Waasiwa Houthi wametumia vita vya Yemen kujiimarisha
Kundi hilo limechukua nafasi ya mapigano yaliyodumu miaka minne nchini humo kati ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran na serikali ya rais Abd-Rabbo Mansour Hadi inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kujaribu kuimarisha nafasi yake katika taifa hilo linalokumbwa na vita.
Kudunguliwa kwa hdege hiyo hapo jana kumekuja wakati kukiwa na mvutano kati ya Iran na Marekani tangu serikali ya rais wa Marekani Donald Trump mwaka uliyopita kujiondoa katika Makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran na kurejesha upya vikwazo dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu.
Maafisa wa Iran kwa upande wake wametangaza vikwazo hivyo kama vita dhidi ya uchumi wake.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema taifa lake huenda likajibu vikali kuhusu sera zisizotabirika chini ya utawala wa rais Trump.
Chanzo: Reuters