1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO, jeshi la Afghanistan wauwa raia wengi zaidi ya Taliban

24 Aprili 2019

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa vikosi vya serikali na vya kimataifa viliuwa raia wengi zaidi kuliko kundi la Taliban nchini Afghanistan katika robo ya kwanza ya mwaka 2019.

https://p.dw.com/p/3HKF2
Afghanistan Security Forces  Soldat Kampfeinsatz gegen Taliban
Picha: Imago/Xinhua

Ripoti hiyo ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) iliyotolewa mjini Kabul siku ya Jumatano (Aprili 24) ilisema kuwa raia 581 waliuawa baina ya tarehe 1 Januari hadi 31 Machi, huku vikosi vya NATO na vya serikali ya Afghanistan vikihusika na vifo 305 kati ya hivyo.

Hata hivyo, waasi walihusika na kuwajeruhi watu wengi zaidi kuliko vikosi vya majeshi ya washirika.

Takribani, nusu ya vifo hivyo vilitokana na mashambulizi ya angani wakati wa operesheni za kuwafuatilia waasi kwenye maficho yao.

Ingawa ripoti hiyo haitaji jina la nchi mahsusi, lakini vikosi vya Marekani hufanya mashambulizi ya anga kila vinapoombwa msaada na jeshi la Afghanistan. 

Zaidi ya asilimi 50 ya raia waliouawa ni wanawake na watoto, alisema mkurugenzi wa haki za binaadamu wa UNAMA, Richard Bennet.

"Mbinu hizi za mashambulizi zimeongeza idadi ya vifo vya raia. Kila kifo, kila majeruhi ni msiba kwa raia. Huu unaendelea kuwa mzozo mbaya kabisa na kuna njia nyingi sana ambazo raia wanauawa na kujeruhiwa." Aliongeza mkurugenzi huyo.

Serikali, Taliban watowa wito kuepusha vifo vya raia

Taliban Extremisten Terroristen Afghanistan
Wapiganaji wa Taliban Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Khan

Mwazoni mwa mwaka huu, Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan alivitaka vikosi vya ardhini kuchukuwa hadhari kubwa wakati wa misako yao ili kuwalinda raia. Waasi wa Taliban, ambao kwa sasa wanadhibiti takribani nusu ya nchi, pia nao wamewataka wapiganaji wao kuepuka kuwalenga raia kwenye mashambulizi yao ya kila siku dhidi ya vikosi vya serikali.

Hii ni mara ya kwanza kwa vifo vya raia vinavyotokana na mashambulizi ya majeshi ya serikali na washirika wake vimezidi vile vinavyosababishwa na maadui zao.

Lakini takwimu hizi zinathibitisha kile ambacho wengine wanakiita kuwa ni tatizo linalozidi kukuwa kwenye vita hivi vya kikatili nchini Afghanistan, ambapo sio tu kwamba raia wanauawa kwenye mashambulizi makubwa ya washambuliaji wa kujitoa muhanga na ya waasi, bali pia kwenye makabiliano kati ya majeshi ya Afghanistan na NATO kwa upande mmoja, na waasi hao kwa upande mwengine.

Msemaji wa jeshi la Marekani, Kanali Dave Butler, alisema usitishaji mapigano ndio njia pekee "ya kukomesha mateso kwa raia." Lakini Taliban imekataa kuzungumza moja kwa moja na serikali ya Ashraf Ghani, licha ya kuwa inafanya mazungumzo na Marekani. 

Mazungumzo yaliyokuwa yaanze mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Qatar kati ya Taliban na watu mashuhuri wa Afghanistan, wakiwemo maafisa wa serikali na wawakilishi wa upinzani, yaliakhirishwa katika dakika za mwisho mwisho, baada ya pande hizo mbili kulumbana juu ya nani anapaswa kushiriki kwenye mkutano huo.

AFP,AP