1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban watangaza kuanza mashambulio ya msimu wa machipuko

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
12 Aprili 2019

Wapiganaji wa Taliban wametangaza kuanza mashambulio mengine katika siku zijazo licha ya  kufanya mazungumzo ya kuleta amani na Marekani yatakayowawakilisha watu wote wa Afghanistan.

https://p.dw.com/p/3GhGU
Taliban Extremisten Terroristen Afghanistan
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Khan

Taliban wametoa tamko hilo refu katika lugha tano kusisitiza kwamba mapigano yataendelea mpaka majeshi yote ya nje yaondoke Afghanistan. Hata hivyo, wapiganaji hao hutoa matamko kama hayo kila mwaka ingawa hawajaacha kushambulia katika misimu ya machipuko na baradi kali.

Katika mashambulio wanayofanya kila siku, Taliban wanawalenga wanajeshi wa serikali ya Afghanistan na askari wa NATO na kusababisha madhara makubwa pia miongoni mwa raia. Jumatatu iliyopita wapiganaji wa Taliban waliwaua askari watatu wa Marekani karibu na kambi kuu ya jeshi la anga la Marekani nchini Afghanistan.

Wapiganaji wa Taliban sasa wanadhibiti maeneo makubwa baada ya vita vya miaka17. Katika wito wao Taliban wamewataka wapiganaji wao wa Mujahedeen kufanya mashambulio kwa moyo wote na dhamira ya kweli kwa kufuata maagizo ya viongozi wao. Pia wamewataka wapiganaji wao waepuke kuwashambulia raia.

Hata hivyo taarifa ya kila mwaka inayotolewa na Umoja wa Mataifa imebainisha kwamba idadi ya vifo ilikuwa ya juu kabisa mwaka uliopita. Lakini kwa mujibu wa ripoti hiyo raia waliuawa pia kutokana na mashambulio yanayofanywa na ndege za Marekani.

Msemaji wa Taliban Sabiullah Mujahid
Msemaji wa Taliban Sabiullah MujahidPicha: picture-alliance/dpa/epa/Stringer

Katika kadhia nyingine, msemaji wa Taliban ameliambia shirika la habari la AP kwamba shirika la msalaba mwekundu na la  afya duniani WHO yamepigwa marufuku kutoa huduma kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Taliban. Hii ni mara ya pili kwa shirika la msalaba mwekundu kupigwa marufuku mnamo kipindi cha hivi karibuni. Msemaji wa WHO Tarik Jasarevic ameelezea wasiwasi wake baada ya marufuku hiyo ya Taliban.

Msemaji wa WHO amesema wataendelea kufanya majadiliano pamoja na viongozi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kutatua marufuku hiyo ya muda mfupi haraka iwezekanavyo, ili waendelee kutoa huduma kwa watu wa Afghanistan. WHO inafanya kampeni ya chanjo nchini Afghanistan, mojawapo ya nchi za mwisho ulimwenguni ambako ugonjwa wa polio bado ni tishio kwa jamii.

Wakati huohuo matayarisho yanaendelea kwa ajili ya mazungumzo ya wajumbe wa Afghanistan tu yatakayofanyika wiki ijayo nchini Qatar ambako Taliban wana ofisi ya uwakilishi wa kisiasa. Baraza kuu la Afghanistan lililoundwa miaka iliyopita kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wapinzani, limelaani tamko la Taliban na limeuliza iwapo wapiganaji hao wanayo dhamira ya kweli ya kufanya mazungumzo ili kuvimaliza vita vya muda mrefu.

Mjumbe wa Marekani anayeshughulikia mgogoro wa Afghanistan Zalmay Khalilzad amewataka Taliban wakubali kusimamisha mapigano na wafanye mazungumzo ya ana kwa ana na wajumbe wa serikali ya Afghanistan. Hata hivyo wapiganaji hao mpaka sasa hawataki kufanya mazungumzo hayo. Lakini wamesema wako tayari kukutana na wawakilishi wa umma wa Afghanistan nchini Qatar na siyo wajumbe wa serikali.

Vyanzo/AP/RTRE/AFP