NASA: Mwaka 2021 ulikuwa na joto kali
14 Januari 2022Kulingana na utafiti wa hali ya joto duniani uliotolewa jana alhamisi na mashirika mawili ya Marekani, mwaka 2021 ulikuwa mwaka wa sita wenye joto zaidi duniani. Data za hivi karibuni zilizokusanywa na shirika la taifa la Marekani linaloshughulikia utafiti wa anga za mbali NASA na taasisi ya bahari na masuala ya Anga NOAA zimesema ongezeko hilo la joto linaongeza athari ya mabadiliko ya tabia nchi.
Soma zaidi:Guterres: Iokoweni dunia ama tutaangamia sote
Mwaka 2021 na mwaka 2018 zote kwa pamoja zilichukua nafasi ya sita, kuwa miaka iliyokuwa na joto kupita kiasi hii ikiwa ni kulingana na shirika la NASA linalotoa data hizo ikilinganishwa na data za miaka 30 ya tafiti zake. Utafiti mwengine tofauti uliofanywa na taasisi ya NOAA ulionyesha kuwa mwaka 2021 ulishuhudia viwango vya joto vya wastani vilivyofikia nyuzi joto 1.51 za Celsius ikiwa juu ya viwango vya karne ya 20, na kuuweka mwaka uliopita katika nafasi ya sita pekee mbele ya mwaka 2018.
Maafisa wa mashirika yote mawili wanasema haya yote ni sehemu ya viwango vya joto vya muda mrefu vinavyoonesha dalili ya kupanda na kuwa vikali zaidi.
Ongezeko la joto duniani ni miongoni mwa madhara ya mabadiliko ya tabia nchi
Takwimu hizi pia zimeuorodhesha mwaka 2013 hadi mwaka 2021 kuwa miongoni mwa miaka 10 iliokuwa na viwango vya juu vya joto tangu mfumo wa kuweka rekodi ulipoanzishwa mwaka 1880. Russell Vose mkurugenzi wa shirika la utafiti wa hali ya joto NOAA, amesema kwa sasa kunashuhudiwa joto kali zaidi kuliko miaka yoyote ile ndani ya miaka 2000 iliyopita.
Russell anasema haya yote yanatokana na ongezeko la gesi zinazozuwia joto kama hewa chafu ya mkaa akisema mwaka 2022 bila shaka utakuwa miongoni mwa miaka iliokuwa na joto jingi.
Soma pia: Ripoti ya IPCC: Dunia yashindwa kudhibiti uzalishaji gesi chafu
Mwaka jana hali ya joto ilikumbwa na unyevuunyevu kutokana na uwepo wa La Nina katika bahari ya pasifiki ya eneo la Mashariki. La Nina ni hali ya asilia ya kupooza maeneo ya pasifiki ya kati inayobadilisha hali ya hewa duniani na kuleta maji ya kina kirefu cha bahari upande wa juu wa bahari, na wanasayansi wanasema mwaka 2021 ulikuwa mwaka wa joto wa La nina kuwahi kurekodiwa.
Kupanda kwa viwango vya joto vinatokana kwa kiasi kikubwa na ongezeko la gesi chafu inayotokana na kupanuka kwa viwanda duniani, ambayo hasa ni matokeo ya shughuli za binadamu. Wanasayansi wanaamini kuwa hali ilivyo sasa viwango vya joto duniani vitapanda zaidi ya nyuzi joto 1.5Celsius ifikapo mwaka 2030.