Myanmar yaanza kuwaachilia huru wafungwa wengine 2,300
30 Juni 2021Mabasi yaliwasafirisha wafungwa walioachiliwa huru kutoka katika gereza lenye sifa mbaya la Insein, ambako tangu asubuhi mamia ya watu walikuwa wakipiga kambi wakisubiri milango ya gereza hilo ifunguliwe kwa wapendwa wao.
Mawakili na marafiki wa baadhi ya wanaharakati na wanahabari waliofungwa wamethibitisha kuachiliwa kwao.
Soma pia: Umoja wa Ulaya umeiongezea vikwazo Myanmar
Zaw Zaw ambaye ni mkuu wa idara ya magereza katika jimbo la Yangon amethibitisha kuwa zaidi ya wafungwa 720 waliachiliwa huru kutoka katika gereza hilo ambalo kwa miongo mingi limekuwa likitumika kuwazuia wafungwa wa kisiasa.
Katika miongo iliyopita ya utawala wa kijeshi, gereza la Insein lilifahamika kama mahali ambako wafungwa waliteswa.
Awali, naibu waziri wa habari Meja Jenerali Zaw Min Tun aliliambia shirika la habari la China Xinhua kwamba wafungwa ambao wameachiliwa huru ni wale ambao hawakujihusisha na vurugu na uhalifu wakati wa maandamano.
Soma pia: Amnesty yaorodhesha ukatili dhidi ya waandamanaji Myanmar
Kulingana na makadirio ya mashirika yasiyo ya kisrikali, watu 883 wameuawa na zaidi ya 6,400 wamekamatwa. Kumekuwa pia na ripoti za watu kuteswa wakati wakihojiwa.
Kundi linalotoa msaada kwa wafungwa wa kisiasa lilisema hapo jana Jumanne kwamba watu 5,224 wako kizuizini kwa kuhusishwa na maandamano dhidi ya jeshi kuchukua madaraka baada ya mapinduzi waliyofanya.
Mwishoni mwa mwezi Aprili, jeshi linaloongozwa na Min Aung Hlaing lilikuwa limewaachilia huru wafungwa 23,000.
Myanmar ilitumbukia katika maandamano na vurugu kupinga mapinduzi ya kijeshi. Jeshi limekuwa likikabili hali kwa kutumia mbinu kandamizi dhidi ya upinzani.
Soma pia: Waandamanaji zaidi wauawa nchini Myanmar
Kiongozi wa kiraia aliyepinduliwa Aung San Suu Kyi mwenye umri wa miaka 76 pamoja na viongozi wengine wa chama chake cha National League for Democracy-NLD wamewekwa kizuizini tangu mapinduzi yalipofanywa.
Suu Kyi anakabiliwa na misururu ya tuhuma ikiwemo ya hongo, kukiuka taratibu za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, kumiliki vijiredio viwili vya mawasiliano kinyume cha sheria na kuchochea watu kukaidi na kufanya uhalifu dhidi ya serikali.
Jeshi la Myanmar lilisema lilichukua madaraka baada ya kukituhumu chama cha Suu Kyi, kushiriki udanganyifu kwenye uchaguzi ambao kilishinda.
(AP, DPA, RTRE)