Mwanamuziki Martelly ashinda uraisi wa Haiti
5 Aprili 2011Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Baraza la Uchaguzi la Haiti yanampa Martelly karibu asilimia 68 ya kura na, hivyo, kumsafishia njia ya kungia ikulu ya taifa hilo masikini lililooko katika Bahari ya Caribbean.
Vifijo na nderemo zilisikika kwenye mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince, mara tu baada ya matangazo kutolewa, huku vijana, ambao wengi wao walimuunga mkono muimbaji huyu wa muziki wa pop, wakiwasha fashifashi.
Akitumia mtandao wa Twitter, Martelly aliwashukuru wapiga kura wake akirudia ahadi yake ya kushirikiana na Wahaiti wote kuijenga nchi yao, ambayo hadi sasa haijatoka kwenye maharibiko ya tetemeko la ardhi la mwaka jana.
"Serikali nitakayoiongoza itaweka umuhimu zaidi katika muundo kuliko fedha. Tunahitaji msaada, tunahitaji mashirikiano, tunahitaji mafunzo, tunahitaji kubadilisha ufahamu wetu, maana kwa sasa tuna akili za kujiharibu wenyewe." Amesema.
Rais asiye na uzoefu wa siasa
Akijuilikana zaidi kwa jina lake la kisanii la "Sweet Micky", Martelly alitumia muda mwingi wa kampeni zake kuahidi mabadiliko kwa mfumo mzima uliopo, ambao unashutumiwa kwa ufisadi na utawala usiojali sheria. Mara nyingi alipanda jukwaani na kutumbuiza kwanza kwa nyimbo zake kabla hajahutubia.
Martelly anatambuliwa kama mwanamuziki mwenye vituko awapo jukwaani, ikiwa ni pamoja na kuvaa nywele za bandia na kuvua nguo zake. Hana uzoefu wowote wa siasa, na hajawahi kushika nafasi yoyote serikalini.
Lakini wachambuzi wanasema kuwa, kwa Wahaiti kumchagua msanii huyu asiye na uzoefu kwenye siasa na kumuwacha Manigat, ni dalili ya kuvunjika moyo kwa wapiga kura wa nchi hiyo na wanasiasa wao.
Licha ya kuwa haya ni matokeo ya awali tu, ambayo yanaweza kupingwa kisheria, lakini tafauti kubwa ya kura kati ya Martelly na Manigat, inaondoa uwezekano wa kuwa na rais mwengine asiyekuwa mwanamuziki Martelly kwa Haiti.
Changamoto kubwa
Sasa Martelly anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuijenga mpya nchi yake, ambayo imeharibiwa kabisa, sio tu na tetemeko la ardhi la Januari mwaka 2010, lililogharimu zaidi ya vifo 300,000, bali pia na uchumi ulioporomoka kabisa. Hadi sasa maelfu ya wahanga wa tetemeko hilo wangali wanaishi kwenye kambi za dharura.
Umoja wa Mataifa na serikali za nchi fadhili, ambazo zimemimina mabilioni ya dola kuijenga nchi hiyo, zinataka kuona uchaguzi huu unatoa serikali iliyotulia na uongozi halali wa kuchukua dhamana ya ujenzi mpya wa nchi.
Marekani yapongeza
Marekani imewapongeza Wahaiti kwa uchaguzi huu, ambao imeuita hatua muhimu sana. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ubalozi wa Marekani nchini Haiti umesema kwamba, tafauti na chaguzi zilizopita, wa mara hii umekuwa na rekodi ndogo kabisa, ya ukiukwaji wa taratibu, na, hivyo kuwataka wale wote watakaolalamikia matokeo yake, kufanya hivyo kwa njia za kisheria na kisiasa.
Vikiwa vinachelea machafuko, vikosi vya Umoja wa Mataifa vimekuwa vikiweka doria kwenye mitaa ya mji mkuu Port-au-Prince na miji mingine muhimu ya nchi hiyo. Baadhi ya maduka bado yamefungwa kwa khofu hiyo hiyo ya machafuko.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji