Idadi ya watu waliokufa kwa kipindupindu Haiti yaongezeka
25 Oktoba 2010Idadi wa watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa kipindupindu nchini Haiti imefikia 250, huku wengine 3,000 wakiwa wameambukizwa ugonjwa huo.
Watu watano wameambukizwa ugonjwa huo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince, lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema wagonjwa hao waligundulika haraka na hatimaye kutengwa.
Mkurugenzi Mkuu katika wizara ya afya nchini Haiti, Gabriel Thimote, amesema ana matumaini kuwa ugonjwa huo unaweza ukadhibitiwa. Thimote amesema hali inaonekana kuimarika, ingawa ugonjwa huo huenda ukafikia katika kiwango cha juu.
Wafanyakazi wa afya wamekuwa wakikabiliana na ugonjwa huo mjini Port-au-Prince nje ya kambi wanakoishi zaidi ya watu milioni moja walioathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea mwezi Januari, mwaka huu.
Shirika la msaada la Oxfam linagawa dawa za kuweka kwenye maji, pakiti za dawa za kuongeza nguvu mwilini na vipande vya sabuni kwa zaidi ya watu 25,000.