1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wandelea kati ya washirika wa Ruto na serikali

14 Septemba 2020

Ulinzi umeimarishwa karibu na kituo kikuu cha polisi mjini Nakuru, baada ya maafisa wa polisi kuzima maandamano yaliyolenga kupinga kile kinachoelezwa kuwa ni kuandamwa kwa washirika wa naibu Rais Wiliam Ruto

https://p.dw.com/p/3iR4U
Afrika Kenia William Ruto Polizeistation
Picha: DW/W. Mbogo

Mbunge wa Kapsaret, Eldoret Oscar Sudi amezuiliwa kwenye kituo hicho cha polisi akisubiri kusomewa mashtaka ya uchochezi na mienendo isiyofaa.

Baada ya wikendi nzima ya kusakwa na maafisa wa usalama mjini Eldoret, Mbunge huyo alijisalimisha kwenye kituo cha polisi cha Langas huko Eldoret jana asubuhi na baadaye kusafirishwa hadi Nakuru anakozuiliwa hadi sasa. Soma pia: Polisi wavunja maandamano ya kumpinga Ruto Kisiii

Wafuasi wa naibu Rais Wiliam Ruto wakiwemo Seneta wa Elgeyo Matrakwet Kipchumba Murkomen, Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, Gavana wa Nandi Stephen Sang miongoni mwa wengine wamewasili katika kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru na wanapiga kambi wakidai haki kwa mbunge Oscar Sudi wanayesema anaandamwa bure ilhali matamshi aliyotoa ni ya ukweli.

Kuna uwepo mkubwa wa maafisa wa polisi karibu na kituo hicho wakishika doria baada ya kutibua maandamano yaliyopangwa kumtetea Sudi. Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri analaani hatua hii. Soma pia: Siasa za Kenya zachukua mkondo wa 2007

Kamata kamata hii ya wafuasi wa naibu Rais William Ruto inaibua taharuki hasa katika maeneo haya ya Bonde la ufa, ikidhihirika wazi sasa kwamba Naibu Rais atawania kiti cha urais kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2022. Kuna hisia miongoni mwa wanasiasa wanaomuunga mkono kwamba baadhi ya vigogo serikalini wanataka kuzima ndoto yake ndio maana wanataka kuzima umaarufu wake. Hata hivyo Ruto mwenyewe ameapa kuhakikisha kwamba wakati huu mwana wa masikini ataliongoza taifa.

Kwa sasa inasubiriwa kuona hatua atakayochukuliwa mbunge Oscar Sudi.

Wakio Mbogho, DW Nakuru.