Polisi wavunja maandamano ya kumpinga Ruto Kisiii
10 Septemba 2020Fujo hizo zimeshuhudiwa siku moja baada ya viongozi kadhaa kuelezea wasiwasi wao kuhusu mazingira ya machafuko yanayojengwa na wanasiasia kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Ziara yake Ruto katika jimbo hilo, aidha inajiri siku mbili tu baada ya kufanya mkutano na baadhi ya viongozi wa jimbo hilo, nyumbani kwake Nairobi.
Vijana waliokuwa wanapinga ujio wa Ruto, walichoma magurudumu kwenye barabara, huku wakiimba nyimbo za kumpinga Ruto. Ruto anaonekana akijipigia debe kabla ya uchaguzi mkuu, baada ya Rais Kenyatta kuonesha wazi kuwa hakuna mgombea ambaye atamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao. Hatimaye Ruto alifika katika jimbo hilo la Kisii na kuandaa mikutano miwili huku akikaribishwa na mamia ya wafuasi wake.
Kumekuwa na minong'ono kuwa waziri wa Usalama wa Taifa, Dkt. Fred Matiang'i ambaye anatokea jimbo la Kisii atawania kiti cha urais ifikapo mwaka 2022. Hatua hiyo yake, haikwenda vizuri na wafuasi wake wanaomuona Ruto kama mpinzani. Jimbo la Kisii lina wapiga kura milioni 1.5, linalowafanya wagombea kiti cha urais kulimezea mate.
Zaidi ya kilomita mia tatu kutoka Kisii, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa anaongoza kikao cha baraza la mawaziri katika ikulu ya Nairobi. Mkutano huo ambao kwa kawaida umekuwa ukifanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la virusi vya corona, leo ulifanyika kwa njia ya ana kwa ana. Mkutano huo umefanyika bila ya kuwepo kwa naibu rais William Ruto ambaye alikuwa katika jimbo la Kisii.
Mkutano huo unafanyika huku baraza hilo la mawaziri likigawanyika. Mkutano huo uliafikia kuwapa wafanyibiashara wa viwango vya chini shilingi bilioni tano ili kuinua uchumi wao. Katika jimbo la Taita Taveta, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alikuwa anaendelea kupigia debe marekebisho ya katiba. Wakazi wengi wakijitokeza kumsikiliza.
Raila amepanga misururu ya mikutano kadhaa kote nchini kupigia debe mikakati ya Maridhiano ya Taifa maarufu kama BBI. Mikutano hiyo ya kisiasa inafanyika licha ya agizo la Rais Kenyatta kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa lengo la kukabiliana na virusi vya corona kwa siku thelathini.
Shisia Wasilwa, DW, Nairobi.