1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msichana wa Kiiran anayedaiwa kupigwa na polisi amefariki

Angela Mdungu
28 Oktoba 2023

Msichana Armita Geravand amefariki dunia mwezi mmoja baada ya kudaiwa kupigwa na polisi wa maadili wa Iran ndani ya treni kwa kukiuka sheria ya uvaaji hijabu. Kifo chake kimeripotiwa na shirika la habari la IRNA.

https://p.dw.com/p/4Y95c
Armita Geravand
Armita GeravandPicha: picture alliance/abaca

Kifo cha Armita Geravand aliyekuwa na miaka 16 kimetokea wakati taifa hilo likiadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha msichana mwingine Mahsa Amini 22, aliyekufa akiwa mikononi mwa polisi mwaka uliopita baada ya kukamatwa kwa kukiuka kanuni za mavazi, hali iliyosababisha maandamano kote nchini humo.

Geravand aliyekuwa chini ya uangalizi maalumu kwa takriban mwezi mmoja alipoteza fahamu baada ya tukio hilo lililogubikwa na utata ndani ya treni lililotokea Oktoba 1.

Soma zaidi: Ni ipi kazi ya Polisi wa maadili wa Iran?

Makundi ya haki za binadamu ndiyo yaliyokuwa ya kwanza kuripoti kisa cha binti huyo kwa kuchapisha picha zake katika mitandao ya kijamii. Picha hizo zilimuonesha akiwa hana fahamu akisaidiwa kupumua kwa mashine hospitali. Mamlaka za Iran hata hivyo, zimekanusha madai kuwa msichana huyo aliumizwa baada ya kukabiliana na maafisa wa polisi waliokuwa zamu kuhakikisha kanuni za Kiislamu za mavazi zinaheshimiwa ndani ya treni za Tehran.

Chanzo cha kifo bado ni utata

Hadi sasa, haijulikani kilichotokea sekunde chache baada ya Armita Geravand kuingia ndani ya treni hiyo. Wakati rafiki wa msichana huyo aliiambia televisheni ya taifa kuwa Geravand alijigonga kichwani akiwa katika kituo cha treni, ripoti ya kituo hicho hata hivyo haikuonesha video yoyote ya ndani ya treni na haikutoa ufafanuzi wa sababu ya kutorushwa kwa sehemu hiyo.

Picha ya CCTV ikionesha wakati Armita Geravand alipotolewa kwenye treni
Picha ya CCTV ikionesha wakati Armita Geravand alipotolewa kwenye treni Picha: Iranian state TV/AP/picture alliance

Treni nyingi za Tehran zina kamera za kufuatilia usalama za CCTV ambazo huangaliwa na wafanyakazi wa maalumu wa usalama. Wazazi wa Armita baada ya tukio hilo walionekana kwenye televisheni ya taifa wakisema kuwa jeraha la mtoto wao huenda lilisababishwa na shinikizo la damu,  kuanguka au yote kwa pamoja.

Soma zaidi: Iran yaanzisha msako wa wanawake wasiofunika vichwa vyao

Wanaharakati wa nje ya Iran wamedai kuwa kuna uwezekano kuwa msichana huyo alisukumwa au kushambuliwa kwa kutokuvaa hijab. Wametaka pia uchunguzi huru ufanywe na ujumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa wa kuchunguza matukio nchini humo wakitolea mfano wa tabia ya kuzishinikiza familia za waathiriwa, na mwenendo wa televisheni ya taifa ya Iran kurusha kauli zao kwa kuwashurutisha.

Nchini humo, wanawake wanalazimika kisheria kufunika vichwa vyao na kuvaa nguo ndefu zisizobana. Watu wanaokiuika sheria hizo hukemewa na umma, hupigwa faini au kukamatwa na polisi. Licha ya sheria hiyo wanawake wanaojitokeza hadharani bila kujifunika wameongezeka katika maeneo kama vile migahawani na kwenye maduka tangu kifo cha Mahsa Amini mwaka uliopita.