1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpatanishi mpya wa Syria kuanza kazi leo

Admin.WagnerD10 Septemba 2012

Mpatanishi mpya wa kimataifa katika mgogoro wa Syria Lakhdar Brahim anaanza rasmi kazi yake leo hii, kwa kukutana na viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pamoja na viongozi wa Misri mjini Cairo.

https://p.dw.com/p/165zF
Lakhdar Brahimi mpatanishi mpya wa Syria
Lakhdar Brahimi mpatanishi mpya wa SyriaPicha: AP

Lakhdar Brahimi aliwasili mjini Cairo jana jioni, akitokea mjini New York na kupitia Paris, Ufaransa. Hatua ya kwanza katika kazi ngumu ya usuluhishi wa mgogoro wa Syria itakuwa mazungumzo anayoyafanya mjini Cairo leo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil al-Arabi, na kisha kuelekea Ikulu ya Misri kukutana na rais wa nchi hiyo Mohammed Mursi. Akiwa mjini Cairo, Brahimi vile vile atazungumza na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Mohammed Kamel Amr.

Majukumu ya kutafuta suluhu la amani katika mgogoro wa Syria yaliangukia mikononi mwa Lakhdar Brahimi, baada ya mpatanishi wa kwanza, Kofi Annan kujiuzulu kutokana na mgawanyiko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro nchini Syria, ambao umekuwa ukimwaga damu nchini humo kwa muda wa miezi 18 iliyopita.

Changamoto ya kuogofya

Brahimi anasema wasyria wenyewe ndio wenye jukumu kubwa kumaliza mgogoro nchini mwao
Brahimi anasema wasyria wenyewe ndio wenye jukumu kubwa kumaliza mgogoro nchini mwaoPicha: picture alliance / dpa

Kuendelea kwa mapambano makali baina ya Serikali ya Rais Bashar al-Assad na waasi kumedhoofisha uwezekano wa kupata mwafaka wa kisiasa kumaliza mgogoro huo, na tayari Lakhdar Brahimi mwenyewe amekiri kuwa na hofu juu ya changamoto inayomsubiri.

''Sina tabia ya kutoa ahadi zenye kupandisha matumaini. Nataka kuwaambia watu wa Syria kwamba wanayo matatizo makubwa, na pia majukumu kama watu wengine. Kuna lawama kwamba hakuna makubwa yanayofanywa kusimamisha mauaji nchini Syria, na kuna ukweli ndani yake. Lakini narudia hili tena kwa watu wa Syria na wote wengine; hakuna kikubwa ninachoweza peke yangu, wao ndio wanaweza kutoa mchango mkubwa.'' Amesema Brahimi.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao nchini Uingereza, watu wapatao 27,000 wamekwishauawa katika mgogoro wa Syria. Makadirio ya umoja wa Mataifa ni kwamba waliokufa ni takribani 20,000.

Mgawanyiko unaendelea

Mpatanishi wa kwanza wa kimataifa kuhusu Syria Kofi Annan alisema alikosa ushirikiano
Mpatanishi wa kwanza wa kimataifa kuhusu Syria Kofi Annan alisema alikosa ushirikianoPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa bwana Brahimi, Ahmad Fawzi amewaambia waandishi wa habari mjini Cairo kwamba tarehe ya mpatanishi huyo kwenda nchini Syria itaamliwa baada ya kukamilishwa kwa agenda ya mikutano yake huko.

Wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea kutafuta suluhisho la amani, nchini Syria kwenyewe mapigano yanaendelea, na idadi kubwa ya watu wameripotiwa kuuawa. Katika juhudi hizo za Kidiplomasia, Iran imetangaza kujiunga na juhudi za Misri, Saudi Arabia na Uturuki, katika mazungumzo ya pande nne kutafakari njia za kutulia ghasia nchini Syria.

Wakati mpatanishi Lakhdar Brahimi akianza rasmi kazi yake, bado kuna mgawanyiko kimaoni katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kumaliza mgogoro wa Syria. Akizungumza nchini Urusi mwishoni mwa juma, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton alisema itakuwa kupoteza muda kuweka azimio jingine la Umoja wa Mataifa, kwa sababu Rais Bashar al-Assad atalikiuka.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman