1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Mazingira waendelea Kanada

Erasto Mbwana2 Desemba 2005

Marafiki wakubwa wa Marekani wameonyesha matumaini yao kuwa wanaweza kuishawishi nchi hiyo yenye wasiwasi kuhusu mbinu mpya za kupambana na kuongezeka kwa ujoto duniani katika mkutano wa Mazingira unaohudhuriwa na Wajumbe kutoka nchi 189 mjini Montreal, Kanada.

https://p.dw.com/p/CHoC
Rais wa Marekani George W. Bush
Rais wa Marekani George W. BushPicha: AP

Marekani, ambayo ni mchafuzi mkubwa wa gesi zinazosababisha kuongezeka kwa ujoto duniani, imeamua kutoshiriki katika mazungumzo yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa katika miaka ijayo kuhusu njia za kupunguza kuongezeka kwa halijoto kali.

Mazungumzo kama hayo yanaungwa mkono na Wajumbe wengi wanao hudhuria mkutano wa hali ya hewa ulioanza mjini Montreal, Kanada Novemba 29 na utakaomalizika Desemba tisa.

Kanada, mwenyeji wa mkutano na nchi za Umoja wa Ulaya, zimesema kuwa zinaweza kuondoa wasiwasi wa Marekani kuwa mazungumzo kama hayo hayatailazimisha kutotekeleza upinzani wake.

Itakumbukwa kuwa Marekani imekataa kutia saini Itifaki ya Umoja wa Mataifa ya Kyoto yenye lengo la kupunguza kuongezeka kwa ujoto duniani.

Afisa mmoja wa Kanada amesema, “Tunafikiri Marekani inaweza kutafuta njia ya kushiriki katika mazungumzo kama hayo.”

Kiongozi wa ujumbe wa Uingereza, ambayo ni Rais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, Bibi Sarah Hendry, amesema, “Tunaamini kuwa tunaweza kuafikiana, maridhiano ambayo yatakuwa ya manufaa kwa pande zote zinazohusika.”

Marekani imeuambia mkutano kuwa haitaki kuzungumzia majukumu mapya. Imesema kuwa inajishughulisha zaidi na malengo ya ndani ya nchi ya kupunguza miali ya sumu na kuwekeza zaidi katika tekinolojia safi kama vile haidrojeni.

Hata hivyo, Kanada na Umoja wa Ulaya zinatumaini kuwa mkutano wa Montreal utazindua njia mbili. Mazungumzo mapya kati ya nchi zilizotia saini Itifaki ya Kyoto kuhusu kifanywe nini baada ya mwaka 2012 na kupanuliwa zaidi kwa mazungumzo kati ya nchi zinazoendelea na Marekani.

Kyoto, kinyume chake, inahitaji mataifa 40 yaliyoendelea kiviwanda kupunguza gesi zinazosababisha ujoto kwa asili mia 5.2 chini ya kiwango cha mwaka 1990 kuanzia mwaka 2008 mpaka 2012.

Rais George W. Bush wa Marekani amejitoa katika mazungumzo hayo mwaka 2001 na kudai kuwa Itifaki ya Kyoto ina bana maendeleo ya kiuchumi.

Walinzi wa Mazingira wanasema kuwa mataifa mengi yanapunguza matumaini ya kuchukuliwa hatua kubwa za kupambana na kuongezeka kwa ujoto duniani kunakosababishwa na uchafu unaotoka viwandani na magari.

Miaka kumi iliyokuwa na joto sana tokea kuanza uwekaji wa takwimu katika miaka ya 1860 ilianza mwaka 1990.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa kuongezeka kwa gesi chafu huenda kukasababisha balaa kubwa la mazingira kama vile vimbunga, ukame na mafuriko.

Isitoshe, milima ya barafu huenda ikayeyuka, vina vya maji ya bahari huenda vikaongezeka na miji iliyoko pwani huenda ikazama na hasa ile iliyoko katika visiwa vya Bahari ya Pasifiki.

Taarifa iliyotolewa na kikundi cha nchi 77 zinazoendelea na China imeyaomba mataifa tajiri kufikiria majukumu mapya ya kupunguza gesi za sumu hata baada ya mwaka 2012 na yakamilishe mazungumzo yao hadi ifikapo mwaka 2008.

Wakati huo huo, Wanaharakati wanaotaka hatua zichukuliwe haraka za kuzuia kuongezeka kwa ujoto duniani wataandamana kesho Jumamosi katika miji ipatayo 40 nchini Marekani.

Maandamano makubwa yatafanywa mjini Montreal, Kanada na katika nchi zipatazo zaidi ya 30 ulimwenguni kote.

Watayarishaji wa Maandamano wanataka kuilazimisha Marekani itie saini Itifaki ya Kyoto iliyobuniwa mwaka 1997 na kuidhinishwa na nchi 140.

Kiongozi wa kikundi kinachoitwa Muungano wa Kupambana na Hali ya Hewa, Ted Glick, amesema, “Hili siyo suala la mazingira peke yake isipokuwa ni suala la kufa na kupona.”