1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mazingira waanza.

3 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CW4D

Bali, Indonesia. Mkutano mkubwa kabisa wa mabadiliko ya hali ya hewa umeanza katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia. Wajumbe kutoka mataifa 180 wamewasili katika mazungumzo hayo yanayosimamiwa na umoja wa mataifa, yenye lengo la kufikia makubaliano ya dunia ifikapo mwishoni mwa mwaka 2009 ambayo yatachukua nafasi ya makubaliano ya Kyoto, ambayo muda wake unamalizika 2012.

Watayarishaji wa mkutano huo wanatarajia kupata ushirikiano na mataifa makubwa yanayotoa kwa wingi gesi zinazochafua mazingira, kama Marekani na China.Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mwenyekiti wa mkutano Yvo de Boer amesema kuwa mada hii ni ngumu lakini inaweza kujadilika.

Katika ujumbe kwa njia ya video kabla ya mkutano huo kuanza , kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuwa nchi yake itakuwa mbele katika uongozi wa ulinzi wa hali ya hewa kwa kutoa mpango ambao utapunguza kwa asilimia 40 utoaji wa gesi za kabon ifikapo mwaka 2020, pamoja na kutanua wigo wa vyanzo vya upatikanaji wa nishati endelevu.