1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mazingira wa rais Bush ni kiini macho

Sekione Kitojo1 Oktoba 2007

Baada ya miaka kadha ya kukanusha , mkutano uliodhaminiwa na Ikulu ya Marekani kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa, umemalizika siku ya Ijumaa huku rais George W. Bush akikiri kuwa ongezeko la ujoto duniani ni suala ambalo halikaniki na binadamu wanahusika na amewataka viongozi wa mataifa kuungana nae mwaka ujao katika mkutano mwingine.

https://p.dw.com/p/CH7Q
Rais Bush akihutubia mkutano wa mazingira mjini Washington.
Rais Bush akihutubia mkutano wa mazingira mjini Washington.Picha: AP

Haielekei iwapo mtu yeyote mwenye mtazamo thabiti atahudhuria mkutano kama huo tena , wakati rais Bush anaendelea kutoa msukumo kwa uamuzi wa binafsi wa upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira , wakati dunia yote , ikiwa ni pamoja na kiasi kikubwa cha sekta ya wanabiashara , tayari wamekwisha sema kuwa ushughulikiaji wa suala hili kwa taratibu hauwezi kukubalika.

Rais Bush anaaminika kwa kiasi kidogo sana kuhusiana na suala la mabadiliko ya hali ya hewa, amesema Chris Flavin , rais wa taasisi ya Worldwatch, kundi lililo na makao yake makuu nchini Marekani linalohusika na mazingira.

Ni maafisa wa ngazi ya kati kutoka mataifa 16, umoja wa Ulaya na umoja wa mataifa walioshiriki katika mkutano huo siku ya Alhamis na Ijumaa.

Flavin ameliambia shirika la habari la IPS kuwa kuna umoja wa hali ya juu kimataifa kuhusiana na haja ya kuweka viwango maalum vya upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Utawala wa rais Bush umekuwa katika mbinyo mkali kutoka jumuiya ya kimataifa, Wamarekani wenyewe, baadhi ya sekta ya wanabiashara nchini Marekani pamoja na kutoka ndani ya chama cha Republican binafsi, kuhusiana na haja ya kulishughulikia suala la mabadiliko ya hali ya hewa, amesema Elliot Diringer, mkurugenzi wa mikakati ya kimataifa katika kituo cha Pew kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, kundi la ulinzi wa mazingira linalofanyakazi kwa ushirikiano na sekta ya mashirika makubwa.

Makampuni mengi yanataka upunguzaji wa gesi hizo unaolazimisha viwango pamoja na mfumo wa biashara ya gesi ya carbon na sheria zilizowazi juu ya ulazima wa upunguzaji huo, Diringer amesema katika mahojiano.

Ameongeza kuwa mkutano huo uliotayarishwa na Ikulu ya Marekani ni mabadiliko tu ya mbinu, na sio mabadiliko ya msimamo.

Baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na maelezo ya hadharani ya kumuunga mkono kiongozi wa umoja wa mataifa kuhusiana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo yalizaa mkataba wa Kyoto. Baadhi ya watu wengine wamesema kuwa mkutano huo wa Ikulu ya Marekani ulikuwa ni jaribio la kuyumbisha mtazamo wa Wamarekani na vyombo vya habari kutoka katika mkutano wa umoja wa mataifa unaohusika na mabadiliko ya hali ya hewa uliofanyika mapema wiki iliyopita, ambapo zaidi ya viongozi wa mataifa 80 waliidhinisha dhana ya makubaliano ya kimataifa baada ya mkataba wa Kyoto unaozuwia utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Ni jaribio la kuondoa njiani hatua za umoja wa mataifa kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa, amesema Lo Sze Ping, mkurugenzi wa kampeni inayofanywa na kundi la Greenpeace nchini China, juu ya mkutano huo wa mjini Washington. Marekani na Australia zinapaswa kuacha kuwaonyeshea vidole wengine na kuchukua hatua, Sze Ping amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, akidokeza kuwa China ina mahitaji ya utumiaji mzuri wa mafuta kwa magari, unaowajibisha matumizi ya nishati endelevu ifikapo mwaka 2020, pamoja na vuguvugu la upunguzaji mwingine wa gesi hizo ambazo zinapita kwa kiwango kikubwa juhudi za Marekani na Australia.