Mkutano wa Mazingira mjini Durban wamalizika kwa mafanikio
12 Desemba 2011Wajumbe kutoka mataifa 194 hatimae walifikia makubaliano na kuondoa hofu iliokuweko kwamba huenda mkutano huo wa Umoja wa mataifa ungeshindwa. Mkataba huo sasa umeuokoa ule mkataba wa Kyoto.
Wiki mbili za majadiliano marefu hatimae zilizaa matunda jana na hivyo mkutano huo wa Umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kumalizika mjini Durban Afrika kusini kwa mafanikio kwa tangazo la mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na suala hilo Bibi Christiana Figueres.Makubaliano yalifikiwa dakika ya mwisho kutokana na muda wa masaa 30 ya nyongeza, uliofuatia wito wa mwenyekiti wake , Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Afrika kusini Naite Nkoana Mashabane ambaye akizungumzia juu ya haja ya kupatikana makubaliano
alisema :
"Nafikiri tumetambua kwamba si barabara. na tusiruhusu kisichokuwa barabara kuharibu kizuri na kinachowezekana ."
Waziri Mashabane alikuwa akitoa wito kwa wajumbe kuzingatia umuhimu wa kuafikiana.
Hivi sasa kile kinachojulikana kama jukwaa la Durban, limefungua njia ya kuanza utaratibu wa kuwa na sera ya dunia juu ya mabadiliko ya tabia nchi, itakayoongoza juhudi za kupunguza utoaji gesi zinazochafua mazingira katika kipindi cha miaka 10 ijayo, ili kiwango cha joto kibakie katika kipimo cha gredi mbili Celsius. Wachambuzi wanasema kutokana na sera ya sasa kiwango hicho cha joto ni katika kipimo cha gredi nne celsius.
Mkataba mpya kwa hivyo unaweka mpango wa mabadiliko ya tabia nchi hadi 2017 au 2020, ambapo sio tu nchi zilizoendelea kiviwanda zitakazotakiwa kuwajibika bali hata nchi zinazoendelea nazo zitakuwa na wajibu wa kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira.
Umoja wa Ulaya kwa upande wake uliungana na wanaharakati duniani kukaribisha mafanikio hayo, lakini ukasema dunia itahitaji mpango mkubwa zaidi kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira, kuliko ilivyokuwa katika mkataba wa awali wa Kyoto.
Licha ya kwamba makubaliano ya Durban si muafaka kabisa lakini ni hatua moja kubwa mbele. Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na mazingira Connie Hedegaard amesema :
"Unapokuwa na tatizo kubwa, Unatpokuwa na tatizo la dunia, tatizo la kimataifa. basi hatua sa hiyari huwa hazitoshi kulitatuwa tatizo hilo."
Mkutano wa Durban ulifikia tamati na kutoa matumaini kutokana na maridhiano hasa kati ya India na Umoja wa Ulaya chini ya usimamizi wa mwenyekiti wa mkutano huo Bibi Mashabane.
Durban imezaa ushirikiana mpya kati ya nchi zinazoendelea na Umoja wa Ulaya katika kukabiliana na ongezeko la ujoto duniani.
Mtaalamu wa Shirika la mazingira la Greenpeace Martin Kaiser amesema,Ni jambo zuri kuona China, India ,Brazil na Afrika kusini zikishirikiana ana hatimae kufanikisha kupatikana kwa mkataba mpya kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Miaka mitano ijayo itatoa sura ya awali ya kule dunia inakoelekea.
Mwandishi: Jeppessen Halle/ ZR/ Moahammed Abdul-Rahman
Mhariri: Othman Miraji