1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa Copenhagen.

8 Desemba 2009

Je, utamalizika bila ya maamuzi wazi ?

https://p.dw.com/p/KxE6
sayari yetu na hali ya hewaPicha: AP

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo, yamechambua mada mbali mbali kama uamuzi wa serikali ya Ujerumani kuwalipa fidia jamaa wa raia walio uwawa katika ile hujuma ya anga ya shirika la NATO huko Kunduz ,Afghanistan, na juu ya mkutano ulioanza jana wa kuzuwia uchafuzi wa hali ya hewa mjini Copenhagen,Denmark.Gazeti la "VOLKSSTIMME" kutoka Magdeburg laandika:

"Kuzuwia uchafuzi wa hali ya hewa ulimwenguni, ndio jukumu kuu uliojitwika mabegani mwake mkutano huo wa Umoja wa mataifa huko Copenhagen.Kwa wiki mbili za mkutano huo,wajumbe 15.000 wamewasili huko....

Isitoshe, zaidi ya viongozi wa dola 100 watahudhuria duru ya mwisho ya mkutano huu.Shabaha ya kikao hiki kikuu, ni kuteremsha kima cha ujoto katika sayari hii kutopindukia nyuzi 2.Lakini maazimio yote yaliopitishwa hadi sasa kuzuwia dhara zinazochafua mazingira ,kwa maoni ya mabingwa wa mazingira hayakutosheleza kukifanya kile hasa kinachobidi kufanywa.

Kwahivyo, kuna fursa mjini Copenhagen mara hii, kwa matarajio yaliokuzwa kabla ya kikao hiki kuyatimiza na kupindukia. Kinacho hitajika hasa, ni kupitisha maazimio yanayo mfunga kila mmoja kuyatekeleza na sio tu kutoa tena porojo tupu ili gharama kubwa zilizotumika kuitisha mkutano huu, si za bure."

Ama gazeti la Kölnische Rundschau linasema kwamba, biashara ya moshi unaochafua mazingira hadi sasa ,haikutimiza matarajio.Sababu yake hasa ni kuwa, hadi wakati huu, hakuna bei maalumu iliowekwa kuwatoza wanaotoa moshi huo unaopaa hewani. Rundschau laongeza:

"Ni pale bei hizo zitakapo wekwa zikilingana na hasara inayo fanywa na moshi huo....ndipo yamkinika maendeleo makubwa yakapatikana.Mkutano wa Copenhagen, kwahivyo, una jukumu la kutoa muongozo na nafasi ya kufanya hivyo, haikuwahi kuwa bora zaidi kama leoi.Kwani, nia ya kisiasa ni kubwa kuliko wakati wowote uliopita. Na ikiwa mnamo miaka 10 ijayo hapatazuka mabadiliko,basi itabakia kuzungumzia misiba tu na porojo mwito uliotolewa kulinda mazingira utageuka porojo tupu."

Nürenmberger Nachrichten, linaandika kwamba, mengi kati ya yale watu wanachukulia ni haki zao za kimsingi, yafaa kuulizwa: Je, ni lazima kila mmojawetu aendeshe motokaa ?

Isipokuwa pakivumbuliwa magari mapya yenye mitambo isiochafua mazingira yetu ndipo yafaa kila mmoja kuendesha.Na hapo, ndipo ilipo fursa kwa viwanda vingi vya magari kuitumia...

Likitukamilishia mada hii ya kikao cha Copenhagen juu ya mazingira, gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE) kutoka Potsdam,laandika:

"Nchi tajiri za magharibi ambazo ndizo chanzo cha uchafuzi wa hali ya hewa ,sasa zinaziuzia nchi masikini mitambo yao ya nishati ya upepo na ya jua .Kwa njia hii, matajiri, wanabakia kuwa matajiri na masikini, wasalia kuwa masikini na dunia inarudi kuwa safi.Ni hali hii ambayo, kundi la nchi 77 la nchi zinazoinukia na zile changa hazikubaliani nayo...."

Mwandishi: Ramadhan Ali/ DPA

Mhariri:Abdul-Rahman