1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa waanza mjini Montreal

Josephat Charo28 Novemba 2005

Kwa mara nyengine tena mataifa wanachama wa umoja wa mataifa yanafanya mkutano wa kilele juu ya kuyalinda mazingira kuanzia hii leo mjini Montreal nchini Canada. Ni kweli kwamba mkataba wa Kyoto, ambao ulisababisha mivutano kati ya mataifa kabla kusainiwa, ulianza kufanya kazi kuanzia mwanzoni mwa mwaka. Hata hivyo lakini, mkataba huo bado hauna nguvu kwani kiwango cha gesi kutoka viwandani kinaendelea kuongezeka.

https://p.dw.com/p/CBJR
Mkutano wa Montreal umeanza leo
Mkutano wa Montreal umeanza leo

Mataifa tajiri yalitakiwa kupunguza kiwango cha gesi zinazotoka viwandani kwa asilimia tano kati ya mwaka wa 1990 na 2010, lakini ukweli uliopo ni kwamba kiwango hiki kimepanda kwa asilimia 10. wataalamu kama vile kiongozi wa taasisi ya utafiti wa mazingira ya Potsdam, bwana Hans Joachim Schellenhuber, anasema ukweli wa mambo ni kwamba kuna miongo kadhaa, au pengine miaka kumi au kumi na tano, ambayo tunaweza kuongeza uwekezaji utakaosaidia kuhifadhi nishati na kupunguza kiwango cha gesi za viwandani ili kuilinda hali ya hewa.

Ili kuzuia kupanda kwa viwango vya joto kwa centigredi mbili kila mwaka, athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinatakiwa kupunguzwa kwa nusu. Kwa sasa jambo hilo haliwezekani chini ya mpango wa kupunguza kiwango cha gesi za viwandani kuingia angani. Mkataba wa Kyoto utafanya kazi mpaka mwaka wa 2012, na mataifa yanayoinukia kiuchumi kama vile India na China yatalazimishwa kupunguza viwango vya gesi za viwandani, jambo ambalo kwa hivi sasa haliko katika mkataba huo wa Kyoto.

Mkutano wa Montreal unafanyika kutafuta njia za kutaka kulitimiza lengo hili lisilojulikana lini litakapofikiwa. Serikali mpya ya Ujerumani inawakilishwa kwa mara ya kwanza na waziri wa mazingira Sigmar Gabriel wa chama cha SPD. Gabriel anataka kulifikia lengo la kuzishawishi Marekani na Australia, ambazo hazikuukubali mkataba wa Kyoto, kushiriki kikamilifu katika siasa ya kuyalinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Wataalamu wanaona mkutano huo ni fursa nzuri kwani hivi majuzi Marekani ilikabiliwa na vimbunga vibaya kuwahi kutokea nchini humo.

Thomas Loster, kiongozi wa wakfu wa München Rück, sehemu ya kampuni la kimataifa la bima, anasema ni lazima tukumbuke jinsi Marekani ilivyokumbwa na vimbunga vibaya katika miaka miwili iliyopita. Tuna hakika kwamba mawazo yanabadilika na kwamba sasa watu wanaona umuhimu wa kuchukua hatua za dharura. Nasubiri kwa hamu kubwa. Anafikiri pia kwamba serikali ya Marekani itabadili msimamo wake na kuufikiria tena uamuzi wake. Mawazo ya wamarekani yanabadilika mioyoni mwao.

Katika mkutano huo wa Montreal waziri Gabriel atatetewa na makundi ya mazingira na kilimo. Hali ya Ujerumani inaweza kuonekana wazi kwani Ujerumani imefaulu kupunguza kiwango cha gesi za viwandani kwa asilimia 19 kuanzia mwaka wa 1990, wakati ambapo moshi wa magari na moshi kutoka kwa makampuni ya kutengeneza stima umeongezeka. Serikali ya sasa ya Ujerumani inatakiwa, kuzifikiria upya siasa za mazingira za serikali iliyopita, na kuliahirisha swala nyeti la hali ya baadaye ya nishati ya atomiki. Katika jambo hili serikali ya mseto inaona kikwazo kikubwa.

Mkutano wa Montreal utakuwa na wakati wa kutosha kujadili maswala madogo madogo, lakini hautarajiwi kuyafikia malengo mapya makubwa. Richard Kinley, kiongozi wa sektretariat ya umoja wa mataifa ya mabadiliko ya hali ya hewa mjini Bonn hapa Ujerumani anasema hakuna uwezekano wa serikali kukubaliana juu ya malengo muhimu katika mkutano wa Montreal. Jambo hilo halitarajiwi, sio lengo, halimo katika ajenda na halitafanyika. Lakini yatakayofanyika Montreal ni muhimu sana, kwani wahusika wa mkataba wa Koyoto watakubaliana juu ya njia za kuuwezesha mkataba huo kutekelezwa.

Kwa utamaduni wake Ujerumani ni taifa linalipigania kuyalinda mazingira. Katika kampeni za uchaguzi wakulima walihimiza jambo hili liachiliwe lakini wanasiasa wa serikali ya mseto bado wamelishikilia.