1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa mataifa ya Ghuba wafanyika Saudia

5 Januari 2021

Viongozi wa nchi za Ghuba wamesaini mpango wa mshikamano na uthabiti baada ya viongozi wa Saudi Arabia na Qatar kukumbatiana hadharani na kuirejesha Doha katika jumuiya hiyo ya kikanda baada ya mzozo wa miaka mitatu.

https://p.dw.com/p/3nXYd
Saudia-Arabien | Begrüßung Mohammed bin Salman und Tamin al-Thani
Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman (kulia) akimlaki Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani kuelekea mkutano wa kilele wa mataifa ya Ghuba.Picha: Bandar Algaloud/Courtesy of Saudi Royal Court/REUTERS

Saudi Arabia iliongoza muungano wa mataifa katika nchi za Ghuba na mataifa mengine kukata uhusiano na njia za usafiri na Qatar kuanzia mwaka wa 2017 kwa madai kuwa Qatar ilikuwa na mahusiano ya karibu sana na Iran na kuunga mkono makundi ya itikadi kali, madai ambayo Qatar iliyakanusha.

Mataifa hayo, pamoja na Oman na Kuwait zilizoongoza mazungumzo ya upatanishi ya pande mbili zilitia saini mpango huo wa maridhiano katika mji wa Al-Ula nchini Saudi Arabia baada ya nchi hiyo kufungua tena jana usiku, mipaka yake ya ardhini, baharini na angani kwa Qatar.

" Kuna haja kubwa leo ya kuunganisha juhudi zetu ili kuliimarisha na kulikuza eneo letu na kupambana na changamoto zinazotuzunguka haswa kitisho cha mpango wa silaha za nyuklia za Iran na mipango yake ya hujuma na uharibifu," alisema mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.

Mapokezi ya kiongozi wa Qatar yaleta msisimko

Katar | Salman bin Abdulaziz in Katar
Mahusiano ya Saudi Arabia na Qatar yalikuwa mazuri kabla ya mwaka 2017Picha: Bandar Algaloud/Saudi Kingdom Handout/AA/picture alliance

Hata hivyo maelezo zaidi ya makubaliano yaliotiwa saini hii leo hayakutolewa kwa umma lakini wachambuzi wameonya kuwa mpango wowote unaweza kuwa katika hatua ya mwanzo na hauwezi mara moja kumaliza mikakati yote iliyochukuliwa dhidi ya Qatar.

Lakini mapokezi mazuri ambayo Mwanafalme Mohammed bin Salman alimpa Emir wa Qatar sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani kwa kukumbatiana katika uwanja wa ndege na kisha kuzungumza kwa furaha ni ishara ya mafanikio makubwa.

Sheikh Tamim anaeitembelea Saudia kwa mara ya kwanza tangua kuanza kwa mzozo baina ya mataifa hayo mawili baadae alichukuliwa na kuelekezwa katika ukumbi wa mkutano mjini Al Ula.

Lakini tunaweza kusema kuna ishara za mwanzo mpya ?

Trump Mideast Plan Muslim Nations
Picha: picture-alliance/AP Photo

Kulingana na profesa wa chuo kikuu cha Kuwait Bader al Saif hizi ni hatua za kwanza au awamu ya kwanza ya maridhiano  ambayo huenda hatua nyengine muhimu zikafuata.

Bader amesema baadhi ya watu huenda wakayapuuzia maridhiano haya lakini kufungua mawasiliano ya moja kwa moja na kuzungumza bila ya kutupiana maneno kati ya Saudi Arabia na Qatar ni hatua moja kubwa iliyopigwa.

Marekani ilizidisha shinikizo la kuja na azimio juu ya kile ambacho Qatar ilikiita mzingiro, ikisisitiza kuwa umoja wa mataifa ya Ghuba ni muhimu ili kumtenga adui mkuu wa Marekani Iran utawala wa rais Donald Trump ukifikia ukingoni.

Jared Kushner mshauri wa rais Donald Trump na mume wa mwanawe alihudhuria mkutano na kushuhudia kusainiwa kwa makubaliano hayo. Tobias Borck, mchambuzi wa familia ya kifalme amesema utawala wa Trump bila shaka sasa utajipiga kifua kudai ushindi katika kurejesha uhusiano kati ya Qatar na Saudi Arabia.