Mkutano kuhusu Syria mjini Munich
11 Februari 2016Ndege za kivita za Urusi na wanajeshi wa Iran wamevisadia vikosi vya rais Bashar al-Assad kuuzingira mji wa Aleppo katika muda wa wiki mbili zilizopita, na kukwamishwa mazungumzo yaliyokuwa yameanza mjini Geneva, na kuitishia Ulaya na mmiminiko mwingine wa wakimbizi. Mamia kwa maelfu ya Wasyria wamekwama katika mpaka wa Uturuki kaskazini mwa Aleppo, ambako waangalizi wanasema watu 500 wameuawa tangu mashambulizi yaanze Februari mosi.
Mjini Munich waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenziwe wa Urusi Sergei Lavrov watakuwa wenyeji wa mkutano wa mawaziri wenzao wa mambo ya kigeni kutoka mataifa 17, katika mkutano unaoelezwa kuwa wakati wa ukweli kwa mchakato wa amani unaoelekea kusambaratika.
Marekani yaionya Urusi kuhusu operesheni zake
Marekani inataka usitishaji mapigano wa mara moja na kuruhusu msaada wa kiutu kupelekwa katika maeneo ya waasi yaliyozingirwa, lakini imetishia kuchukuwa hatua nyingine ambazo hazikubainishwa mara moja, iwapo mazungumzo ya Munich yatashindwa, wakati ambapo mzozo ukizidi kati yake na Urusi kuhusiana na kampeni yake ya angani.
Waziri Kerry anesema, ''Urusi inahitaji kuchangia pakubwa njia za kuendeleza uwezo wa wapinzani na wengine kuja kwenye meza ya mazungumzo na kuweka mazingira ambamo unaweza kuwa na mazungumzo.'' Waziri ameendeea kueleza kuwa Urusi imelifanya hilo kuwa gumu katika siku zilizopita, hivyo wanakwenda kwenye mkutano huu mjini Munich tukiwa na matumaini makubwa kwamba huu utakuwa wakati wa kujua mengi na tunahitaji kuchukuwa hatua haraka.
Mjumbe maalumu wa Marekani katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu IS, Brett McGurk, alisema kampeni ya mashambulizi ya Urusi ilikuwa inalisaidia moja kwa moja kundi hilo. Wakati Moscow imeahidi kuja na mapendekezo mapya ya kuufufua mchakato wa amani mjini Munich, Urusi na Iran zinaendelea kusisitiza kuwa waasi mjini Aleppo ni magaidi kama walivoy IS, na kwamba hakuwezi kuwa na muafaka hadi washindwe kijeshi.
Waasi waapa kuyapa kisogo mazungumzo
Waasi wanasema hawatarudi kwenye mazungumzo hayo ya Geneva yaliyopangwa kuanza tena Februari 25 hadi serikali ikomesha kuzingira miji yao na mashambulizi ya angani. Urusi imependekeza machi mosi kama siku ya kuanza usitishaji mashambulizi, lakini Marekani imepinga hatua hiyo ikisema itaupa utawala wa Bashar al-Assad muda wa wiki tatu zaidi kuendelea kuwaangamiza raia.
Wachambuzi wanaona matumaini madogo ya kusuluhisha tofauti za kimsingi, na idadi inayoongezeka ya waangalizi wanasema Urusi imenufaika na machafuko yaliyosababishwa na vita hivyo, hasa mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya.
Mtafiti wa Chuo kikuu cha Oxford Kooert Debeuf, aliliambia shirika la ushauri la Carnegie, kuwa lengo la rais Putin ni kuyavuruga na kuyadhofisha mataifa ya Magharibi, na kukomesha mvuto wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya NATO kwa mataifa anayoyachukulia kuwa sehemu ya eneo la ushawishi wa Urusi.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo