Kerry, Lavrov wenyeji wa mkutano wa Syria Munich
11 Februari 2016Ndege za kivita za Urusi na wanajeshi wa Iran wamevisadia vikosi vya rais Bashar al-Assad kuuzingira mji wa Aleppo katika muda wa wiki mbili zilizopita, na kukwamishwa mazungumzo yaliyokuwa yameanza mjini Geneva, na kuitishia Ulaya na mmiminiko mwingine wa wakimbizi.
Mamia kwa maelfu ya Wasyria wamekwama katika mpaka wa Uturuki kaskazini mwa Aleppo, ambako waangalizi wanasema watu 500 wameuawa tangu mashambulizi yaanze Februari mosi.
Mjini Munich waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenziwe wa Urusi Sergei Lavrov watakuwa wenyeji wa mkutano wa mawaziri wenzao wa mambo ya kigeni kutoka mataifa 17, katika mkutano unaoelezwa kuwa wakati wa ukweli kwa mchakato wa amani unaoelekea kusambaratika.
Suala kuu ni usitishwaji mapigano
Marekani inataka usitishaji mapigano wa mara moja na kuruhusu msaada wa kiutu kupelekwa katika maeneo ya waasi yaliyozingirwa, lakini imetishia kuchukuwa hatua nyingine ambazo hazikubainishwa mara moja, iwapo mazungumzo ya Munich yatashindwa, wakati ambapo mzozo ukizidi kati yake na Urusi kuhusiana na kampeni yake ya angani.
"Hakuna shaka...kwamba shughuli za Urusi mjini Aleppo na katika kanda nzima hivi sasa zinafanya vigumu zaidi kuweza kuja pamoja kwenye meza ya mazungumzo, na kuweza kuwa na mazungumzo ya kweli," alisema Kerry mapema wiki hii.
Mjumbe maalumu wa Marekani katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu IS, Brett McGurk, alisema kampeni ya mashambulizi ya Urusi ilikuwa inalisaidia moja kwa moja kundi hilo.
Urusi, Iran zinasema waasi wote ni magaidi
Wakati Moscow imeahidi kuja na mapendekezo mapya ya kuufufua mchakato wa amani mjini Munich, Urusi na Iran zinaendelea kusisitiza kuwa waasi mjini Aleppo ni magaidi kama walivoy IS, na kwamba hakuwezi kuwa na muafaka hadi washindwe kijeshi.
Waasi wanasema hawatarudi kwenye mazungumzo hayo ya Geneva yaliyopangwa kuanza tena Februari 25 hadi serikali ikomesha kuzingira miji yao na mashambulizi ya angani. Urusi imependekeza machi mosi kama siku ya kuanza usitishaji mashambulizi, lakini Marekani imehoji hatua hiyo ikisema itaupa utawala wa Bashar al-Assad muda wa wiki tatu zaidi kuendelea kuwaangamiza raia.
Wachambuzi wanaona matumaini madogo ya kusuluhisha tofauti za kimsingi, na idadi inayoongezeka ya waangalizi wanasema Urusi imenufaika na machafuko yaliyosababishwa na vita hivyo, hasa mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya.
Mtafiti wa Chuo kikuu cha Oxford Kooert Debeuf, aliliambia shirika la ushauri la Carnegie, kuwa lengo la rais Putin ni kuyavuruga na kuyadhofisha mataifa ya Magharibi, na kukomesha mvuto wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya NATO kwa mataifa anayoyachukulia kuwa sehemu ya eneo la ushawishi wa Urusi.
Pamoja na hayo, wachambuzi pia wanasema kuna ukomo kwa kiasi gani mashambulizi ya angani ya Urusi yanaweza kufanikiwa, hasa wakati ambapo waasi -- ambao wanaungwa mkono na Saudi Arabia na mataifa mengine ya Ghuba -- wanajichimbia zaidi katika vita vya mjini.
Dhamira ya Marekani yahojiwa
Wengi pia wameikosoa Marekani kwa kutofanya vya kutosha kuwasaidia waasi. Hata waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa anaemaliza muda wake Luarent Fabius, hakuweza kuficha kuvunjwa kwake moyo wakati akitangaza hatua yake ya kujiuzulu siku ya Jumatano akisema: "Hupati hisia kwamba kuna dhamira ya kweli kwa Marekani nchini Syria.
Marekani imekuwa ikisita kujiingiza katika vita nyingine baada ya utata wa Afghanistan na Iraq, na imejikita zaidi kwenye mapambano dhidi ya IS kuliko kushiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya utawala wa Syria na waasi.
"Marekani imeachana na wazo la kumpindua Assad," alisema Camille Grand, kutoka taasisi ya utafiti wa kimkakati mjini Paris. "Kerry anaonekana yuko tayari kukubali chochote kitakachosaidia kutatuta mgogoro huo.....kwa sababu lengo lao ni kudhibiti kupanuka kwa IS."
Joseph Bahout, mtaalamu wa muda katika taasisi ya Carnegie ya mjini Washington, alisema Marekani imejipotezea uaminifu baada ya miaka miwili ya majadiliano yaliyoshindwa.
"Hakuna kinachotarajiwa kutoka kwa Wamarekani ... wanasema kitu kimoja hadharani, na kingine faraghani," aliliambia shirika la habari la AFP. "Mjini Munich, wanataka kukubaliana juu ya usitishwaji mapigano ambao hautatekelezwa kwa sababu Warusi wataendelea kuwashambulia "magaidi."
Ushirikiano wa Marekani na Wakurd
Mgogoro huo unazidishwa ugumu na ushirikiano unaozidi kuwa wa karibu kati ya Marekani na wapiganaji wa Kikurd katika mapambano dhidi ya IS, hatua iliyoiweka katika msuguano na mshirika wake katika NATO, Uturuki, ambayo inapambana na waasi wa Kikurd wanaotaka kujitenga.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikosoa vikali ushirikiano wa Marekani na Wakurd siku ya Jumatano, akisema ulikuwa unaigeuza kanda hiyo katika dimbwi la damu.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo