1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu Mali wafanyika leo Brussels

Saumu Ramadhani Yusuf5 Februari 2013

Serikali mbalimbali duniani na mashirika ya kimataifa wanakutana leo mjini Brussels, Ubelgiji kujadiliana namna ya kutafuta njia za kuisaidia Mali kijeshi na kifedha pamoja na kukuza demokrasia nchini humo.

https://p.dw.com/p/17Y9o
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki MoonPicha: DW

Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na kukifadhili, kukipatia vifaa pamoja na mafunzo, kikosi cha AFISMA chenye wanajeshi 8,000, ambacho kinatarajiwa kuchukua operesheni za kijeshi za Mali kutoka kwa Ufaransa.

Mbali na masuala hayo, wajumbe wa mkutano huo wa kundi la kuisaidia Mali lililoundwa mwaka uliopita, watajadiliana kuhusu mchakato wa kisiasa nchini humo.

Afisa wa Umoja wa Ulaya amesema katika upande wa mchakato wa kisiasa wajumbe watajadili namna ya kuisaidia Mali kufanya uchaguzi ambao rais wa mpito wa Mali, Dioncounda Traore amesema unaweza ukafanyika mwezi Julai mwaka huu.

Umoja wa Ulaya wafikiria msaada wa haraka

Umoja wa Ulaya unafikiria kutoa haraka kiasi cha Euro milioni 250 za misaada ya maendeleo ambazo ilizizuia baada ya kufanyika mapinduzi mwezi Machi, mwaka uliopita.

Maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya
Maafisa waandamizi wa Umoja wa UlayaPicha: AFP/Getty Images

Umoja huo umesema uko tayari pia kuwasaidia waangalizi wa haki za binaadamu watakaokwenda kutafuta ushahidi kuhusu ukiukwaji wa haki za binaadamu unaodaiwa kufanywa na waasi pamoja na wanajeshi wa Mali.

Wanadiplomasia wamesema kuwa nchi 16 wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na Norway zimeahidi kupeleka timu ya watu 250 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la Mali.

Mkutano huo unahudhuriwa na Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na mashirika ya misaada.

Biden aunga mkono takwa la Ufaransa

Ama kwa upande mwingine, Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden ameunga mkono pendekezo la Ufaransa la kutaka kukabidhi haraka operesheni za kijeshi nchini Mali kwa vikosi vya Afrika.

Hayo ameyaeleza mjini Paris, Ufaransa baada ya kukutana na Rais Francois Hollande, ambapo ameongeza kusema kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kukifanya kikosi hicho cha Afrika kama kikosi rasmi cha kulinda amani nchini Mali, mpango ambao maafisa wa umoja huo wanasema uko katika mchakato.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden
Makamu wa Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: picture-alliance/dpa

Ufaransa ina hamu ya kukabidhi operesheni za kijeshi nchini Mali kwa wanajeshi wapatao 8,000 wa Afrika walioahidiwa kupelekwa nchini humo baada ya kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa. Kikosi hicho cha AFISMA bado kinapeleka wanajeshi wake taratibu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius amesema wanataka kukabidhi operesheni hizo kwa AFISMA hasa katika miji ambayo tayari imekombolewa. Akiwa ziarani nchini Mali, mwishoni mwa juma lililopita, Rais Hollande aliahidi kutoiacha Mali ikiwa katika machafuko.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Daniel Gakuba