Kambi za waasi zashambuliwa Mali
4 Februari 2013Akizungumza kupitia radio moja ya Kifaransa, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Laurent Fabius, amesema usiku kucha kuamkia leo ndege za kivita zimeshambulia mkoa wa Kidal, uliyopo mpakani mwa Mali na Algeria. Amesema hatua hiyo ni moja kati ya malengo makubwa ya kuweza kukata uwezo wa kujipatia mahitaji yao muhimu kwa kundi hilo ambalo lilidhibiti sehemu kubwa ya eneo hilo na kushinikiza sheria kali kwa wakazi wa maeneo hayo.
Aidha Fabius amesema kwa mashambulizi hayo waasi hao hawawezi kuendelea kudumu kuishi kwa muda mrefu katika eneo hilo, labda wawe na hazina mpya ya mahitaji yao. Ufaransa iliingia nchini Mali, Januari 11 kwa lengo la kuwazuia kusonga mbele kundi la waasi la Ansar Dine lenye mafungamano na al-Qaida.
Fabius amerejelea msimamo wa nchi yake wa kutaka jeshi la Afrika kuchukua haraka kwa kadri iwezekanavyo dhamana ya ulinzi katika mji wa kihistoria wa Timbuktu. Kwa sasa, Ufaransa inadhibiti mji huo na mingine kadhaa tangu ianze operesheni hiyo.
OIC kuzungumzia ghasia za Mali
Wakati mapigano yakiendelea nchini Mali, viongozi wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiislamu, OIC, wanatarajiwa kukutana mjini Cairo, Misri, ambako pamoja na mgogoro wa Syria, suala la Mali litapewa nafasi. Taarifa zinaeleza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo wanaanza kikao cha maandalizi leo hii. Mkutano huu mkubwa utawakutanisha viongozi 26 kati ya mataifa 57 ya OIC.
Rais Mohamed Morsi wa Misri safari hii anatarajiwa kuchukua uongozi wa umoja huo ambao kwa kawaida nafasi yake inatolewa kwa zamu kwa nchi wanachama. Katibu Mkuu wa OIC, Ekmeleddin Ihsanoglu, amesema mkutano huu wa sasa ulipaswa kufanyika mwaka 2011 lakini uliaharishwa baada ya kutokea vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya Kiarabu na kuwaondoa watawala wanne wa kiimla akiwemo Hosni Mubarak wa Misri.
Mwanadiplomasia huyo wa zamani ya Kituruki amesema mkutano huo wa kilele utajadili migogoro mikubwa katika mataifa ya Kiislamu. Aidha ameonesha kusikitishwa kwake na migogoro sambamba na kasi ya vikundi vyenye misimamo mikali ya Kiislamu ukiwemo huu unaofukuta sasa wa Mali. Tofauti za sera za mambo ya nje na kusaidiana kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo wa kilele wa siku mbili.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef