1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mkataba wa usafirishaji nafaka za Ukraine waongezwa siku 60

14 Machi 2023

Urusi imeafiki usiku wa jana kuongeza muda wa siku 60 pekee wa kuendelea kwa makubaliano ya usafirishaji nafaka za Ukraine. Hayo yanajiri wakati mapigano makali yakiendelea huko Bakhmut.

https://p.dw.com/p/4OdJ1
BdTD | Türkei
Picha: Yasin Akgul/AFP

Taarifa hiyo ya kuongeza muda wa siku 60 kwa  mkataba huo wa usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi,  ilitolewa na Naibu Waziri wa mambo ya Nje wa Urusi Sergui Vershinine. Serikali mjini Kyiv imeikosoa hatua hiyo lakini haikukataa pendekezo la Moscow .

Umoja wa Mataifa na Urusi zilianza jana mjini Geneva nchini Uswisi, mazungumzo ya kufufua makubaliano hayo ambayo yamesaidia kupunguza mgogoro wa chakula duniani uliochochewa na hatua ya Urusi kuivamia Ukraine, na hivyo kuzuia usafirishaji wa nafaka zake.

Mkataba huo uliosainiwa kwa mara ya kwanza mwezi Julai mwaka 2022 na ambao ulifikiwa kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa na Uturuki, ungefikia kikomo Jumamosi ijayo. Kulingana na Umoja wa Mataifa, makubaliano hayo yaliwezesha usafirishaji wa zaidi ya tani milioni 24.1 za  nafaka kupitia Bahari Nyeusi.

Urusi imekuwa ikihimiza pia kuondolewa vikwazo katika usafirishaji wa bidhaa zake za nafaka na mbolea na imekuwa ikilalamika mara kwa mara kushindwa kuuza bidhaa hizo kwenye soko la kimataifa kutokana na vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi.

Soma pia: Urusi yarudi katika mkataba wa kusafirisha nafaka za Ukraine

Ukraine-Krieg | Abkommen über Export von ukrainischem Getreide
Waziri wa Miundombinu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar wanahudhuria hafla ya kutia saini mpango wa usafirishaji salama wa nafaka na vyakula kutoka bandari za Ukraine, Istanbul, Julai 22, 2022. Picha: OZAN KOSE/AFP

Umoja wa Mataifa umebaini leo kuwa kuendelea kwa mkataba huo ni muhimu kwa usalama wa chakula duniani. Wito kama huo ulitolewa mapema jana na Spika wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola:

"Vita hivi vya uchokozi vimeathiri pia usalama wa chakula duniani. Sote tunafahamu athari mbaya zinazoweza kutokea, hususan njaa ulimwenguni ikiwa usambazaji wa chakula utadhoofishwa. Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi ulipelekea mamilioni ya watu kupata chakula na vifaa muhimu kutoka Ukraine. Hali ni ya dharura na ya kutisha."

ICC kuanza kuwashitaki maafisa wa Urusi

Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC inatarajiwa kuanza kutoa waranti wa kukamatwa kwa maafisa wa Urusi, katika kile kinachotazamiwa kuwa kesi za kwanza za uhalifu wa kivita tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Naibu Spika wa Bunge la Urusi Konstantin Kosachyov amesema ICC haina mamlaka juu ya Urusi huku akisema kuwa Mahakama hiyo ni chombo cha ukoloni mamboleo kinachoongozwa na Mataifa ya Magharibi. Moscow itapinga kukamatwa kwa maafisa wake lakini mashtaka hayo ya kimataifa yataimarisha hatua za kuitenga Urusi kidiplomasia.

Soma pia:Urusi na Ukraine zatia saini mkataba wa kihistoria na Umoja wa Mataifa na Uturuki 

Wakati vita vikiendelea, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema mustakabali wa nchi yake utategemea matokeo ya mapigano huko Bakhmut na eneo la mashariki linalokumbwa na vita la Donetsk huku akiapa kuviangamiza vikosi vya Urusi huko Bakhmut.