1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya usafirishaji nafaka za Ukraine kusainiwa leo

22 Julai 2022

Uturuki imesema leo kuwa Urusi na Ukraine zinatarajia kutia saini makubaliano ya kuruhusu kusafirisha tena nafaka kupitia Bahari Nyeusi, na hivyo kuongeza matumaini ya kupungua mgogoro wa kimataifa wa chakula.

https://p.dw.com/p/4EVfo
Ukraine Transport von Getreide
Picha: STR/NurPhoto/picture alliance

Ukraine na Urusi, ambao ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa nafaka duniani, hawakuthibitisha mara moja taarifa hiyo iliyotolewa jana Alhamisi na ofisi ya rais wa Uturuki. Lakini katika video ya usiku wa kuamkia leo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alidokeza kuwa bandari zilizopo kwenye Bahari Nyeusi nchini mwake zinaweza kufunguliwa hivi karibuni.

Taarifa kamili za utiaji saini makubaliano hayo ya kuruhusu tena usafirishaji wa nafaka za Ukraine hazikuwa wazi mara moja, ingawa ofisi ya Rais wa Uturuki imefahamisha kuwa utiaji saini huo unatarajiwa mchana wa leo. Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikuwa safarini kulekea nchini Uturuki.

Soma zaidi: UN: Tunatarajia bidhaa zitaanza kupita Bahari Nyeusi

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amesema makubaliano hayo ni muhimu sana.

"Tunachojaribu kufanya ni kuwa na makubaliano ambayo yataruhusu chakula na mbolea ya Ukraine na Urusi kufikia soko la kimataifa. Kama unavyojua, tumeelezea kwa miezi mingi jinsi shida ya chakula duniani ilivyo mbaya. Na hii ni sehemu kubwa ya mgogoro huo.Kwa hivyo ikiwa tunaweza kutatua hili, tunaweza kuokoa maelfu au hata mamilioni ya watu kutokana mfumuko wa bei ya chakula iliyo nje ya uwezo wao."

Soma zaidiUrusi yataka UN kuingilia mazungumzo ya nafaka

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24 na kutokana na vizuizi vya Urusi katika bandari za Ukraine pamoja na vikwazo vya mataifa ya Magharibi kwa Urusi, kulishuhudiwa duniani kote matatizo ya ugavi na mfumuko wa bei ya chakula na nishati.

Indonesien | Russischer Außenminister Sergej Lawrow beim G20 Gipfel
Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Picha: Anton Raharjo/AA/picture alliance

Urusi yakanusha kuchochea mgogoro wa chakula duniani

Kabla ya kuanza safari kuelekea barani Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema Urusi haichochei mzozo wa chakula duniani na kuwa itaendelea ugavi wa chakula na usafirishaji wa nishati, kwa kuheshimu mikataba ya kimataifa. Lavrov ameendelea kusema kuwa propaganda za Ukraine na mataifa ya Magharibi kwamba Urusi inasababisha njaa ulimwenguni hazina msingi kabisa, na kuwa matatizo yalianza wakati wa janga la Covid-19.

Wakati uvamizi wa Urusi ukiendelea nchini ukraine, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limelishtumu Jeshi la Urusi kwa kutekeleza mateso, kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria na kuwatokomeza kusikojulikana raia katika maeneo yanayokumbwa na vita kusini mwa Ukraine.      

Yulia Gorbounova, mtafiti wa Ukraine katika shirika hilo la HRW, amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema,Vikosi vya Urusi vimegeuza maeneo yaliyokaliwa ya kusini mwa Ukraine kuwa dimbwi la hofu na machafuko makubwa.

(RTRE,DPAE, AFP)