1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkakati wa Bush kuhusu mazingira

P.Martin1 Juni 2007

Rais George W.Bush wa Marekani,amependekeza mkakati mpya wa kushirikiana na mataifa mengine kwa azma ya kuanzisha mfumo mpya kuhusu njia za kupunguza gesi zinazoathiri mazingira.

https://p.dw.com/p/CB3p
Rais George W.Bush akieleza mkakati mpya kupambana na ogezeko la joto duniani
Rais George W.Bush akieleza mkakati mpya kupambana na ogezeko la joto dunianiPicha: AP

Rais Bush alitoa pendekezo hilo alipozungumza mjini Washington ikiwa ni kabla ya mkutano wa kilele wa mataifa yaliostawi kiviwanda G-8. Mkutano huo utafanywa juma lijalo katika mji wa Heiligendamm nchini Ujerumani.Hadi hivi sasa,Bush alijitenga kabisa na jitahada za jumuiya ya kimataifa za kuweka viwango maalum katika juhudi za kupunguza gesi zinazotoka viwandani na kuathiri hali ya hewa duniani.Marekani imekataa kutia saini Mkataba wa Kyoto ulioweka masharti ya kupunguza uzalishaji wa kaboni dayoksaidi ambayo huongeza ujoto duniani.Sababu mojawapo kubwa iliyotolewa na Marekani ni kwamba hata mataifa mengine makuu yanayoinukia kiuchumi,hayakutia saini Mkataba wa Kyoto utakaomalizika mwaka 2012.Sasa lakini yadhihirika kuwa Bush ndio anataka kushika bendera kuongoza vita dhidi ya ongezeko la joto duniani.Bush alisema hivi:

“Hadi ifikapo mwisho wa mwaka ujao,Marekani na madola mengine yataweka malengo ya muda mrefu kupunguza uzalishaji wa gesi zinazoathiri mazingira.Ili kuweza kutekeleza malengo hayo Marekani itakutana na nchi ambazo huzalisha sehemu kubwa ya gesi hizo,ikiwa ni pamoja na mataifa yanayoinukia kiuchumi kama India na China.”

Kwa maoni ya Bush mataifa makuu 15 yanayochafua mazingira zaidi duniani yaanze kukutana majira ya mapukutiko baadae mwaka huu.

Lakini wito huo wa Bush ni kinyume na matumaini ya Ujerumani kuwa makubaliano kuhusu njia za kupambana na tatizo la ongezeko la joto duniani yatatiwa saini kwenye mkutano wa G-8 utakaofanywa juma lijalo mjini Heiligendamm.

Juu ya hivyo,hatua ya Bush imekaribishwa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani,nchi ambayo hivi sasa imeshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya na ni mkaribishaji wa mkutano wa G-8. Hata Waziri Mkuu wa Japan,Shinzo Abe hii leo alisifu pendekezo la Rais Bush la kutaka kuanzisha mfumo mpya wa kimataifa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Amesema, anaamini kuwa Marekani hatimae inatia maanani suala la ongezeko la joto duniani.

Lakini kwa maoni ya Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya,Jose Manuel Barosso mapendekezo mapya ya Bush kuhusu ulinzi wa mazingira,hayaendi umbali wa kutosha.Amesema,Marekani kama mzalishaji mkuu wa gesi zinazochafua mazingira,ingechukuwa dhamana kubwa zaidi.