1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliofariki ajali ya Kariakoo waagwa

18 Novemba 2024

Miili ya watu waliokufa baada ya jengo moja kuanguka katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imeagwa leo Jumatatu katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

https://p.dw.com/p/4n7Is
Tanzania Dar es Salaam |
Jengo lililoporomoka katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania Picha: Gidulaus Amosi/AFP

Miili ya wahanga 15 wa tukio hilo ilifikishwa kwenye viwanja hivyo ikiwa imebebwa na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi kwa ajili ya kuagwa kabla ya kuzikwa, kufuatia kisa hicho kilichotokea Novemba 16, 2024.

soma zaidi:Jengo laporomoka na kuuwa kadhaa Kariakoo Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa nchini Tanzania Kassim Majaliwa ameongoza shughuli ya kuaga miili hiyo, iliyohudhuriwa na waombolezaji waliojitokea zwa wingi, na waliogubikwa na huzuni kubwa.

Juhudi za uokozi zimeendelea ili kuwaokoa waliokwama kwenye kifusi cha jengo hilo wakati ndugu, jamaa na marafiki wakiendelea kupokea  jumbe mbalimbali za wenzao walionaswa kwenye kifusi wakiomba msaada na baadhi wakiwaaga wakiashiria kuwa pengine hawataonana tena.

Rais Samia Suluhu Hassan aagiza uchunguzi zaidi wa majengo

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameagiza timu ya uokoaji iongezwe katika eneo hilo la Kariakoo ili kuharakisha zoezi hilo na kufanikisha kuwaokoa.

Idadi ya waliokwama haikuwa wazi, lakini baadhi ya watu wameviambia vyombo kadhaa vya habari nchini humo kwamba wamepoteza mawasiliano na jamaa zao ambao wanaamini bado wako chini ya jengo hilo lililoanguka.

Zaidi ya watu 80 wamekwishaokolewa kutoka chini ya jengo hilo la ghorofa nne lenye maduka. Kulingana na Rais Suluhu siku ya Jumapili, watu 26 walikuwa wanapatiwa matibabu hospitalini na serikali ikaahidi kulipia gharama za tiba na mazishi.

Samia Suluhu Hassan | Rais wa Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika tathmini ya majengo yaliyoko Kariakoo jijini Dar es Salaam baada ya kisa cha kuporomoka za jengoPicha: Daniel Pier/NurPhoto/picture alliance

Kiongozi huyo aidha aliagiza majengo yote yaliyoko kwenye eneo la Kariakoo kufanyiwa tathmini. Eneo hilo linasifika kwa biashara mbalimbali.

Baadhi ya wataalamu wa majenzi wamekuwa wakikosoa ujenzi holela

Mamlaka nchini Tanzania zinaanza kuchukua hatua kuyamulika maghorofa yaliyoko katika eneo hilo la Kariakoo.

Baadhi ya wataalamu wa majenzi na wafanyabiashara wamekuwa wakikosoa jinsi ujenzi holela unafanywa ,katika eneo hilo huku wengine wakitaja ripoti kadhaa za nyuma ambazo zilibainisha kuhusu ujenzi holela usiozingatia utalaamu.

Vitendo vya rushwa, kukosa uwajibikaji pamoja na uzembe kutoka kwa mamlaka za kiutendaji ni baadhi ya hoja zinazoibuliwa wakati huu ambako mjadala wa  majengo katika maeneo hayo ikiendelea kuwa bado inayozingatiwa na wengi.

Mtaalamu wa usanifu majenzii Mark Shija amesema ingawa bado ni mapema kubaini chanzo cha kuanguka kwa jengo hilo, lakini hali ya kujirudia mara kwa mara kwa matukio ya aina hiyo inaacha maswali mengi kwa mamlaka na wataalamu wenyewe.

Soma pia:Serikali ya Tanzania yaunda tume na wafanyabiashara