Mgomo wa wafanyakazi kulemaza shughuli za maisha Ufaransa
7 Machi 2023Vyama hivyo vinasema kuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64, kunakoambatana na muda zaidi wa kuchangia katika fuko la pensheni kutaathiri vibaya mamilioni ya wafanyakazi.
Laurent Berger, Katibu Mkuu wa CFDT- mojawapo ya vyama vinavyoratibu mgomo huo, amesema wataweka shinikizo hadi pale suluhisho la kisiasa litakapopatikana.
"Hili ni tatizo la haki ya kijamii, la kukosa usawa. Ni tatizo la kutozingatia hali halisi ya kazi na malalamiko ya wafanyakazi. Je, ni sahihi kulipuuza kama suala la kisiasa litakalotatuliwa bungeni? Hapana. Leo hii kuna vuguvugu la kijamii ambalo litazidi kukuwa kesho, na tunahitaji jibu la kisiasa.''
Mpango huo wa mageuzi katika mfumo wa pensheni ulikuwa kauli mbiu ya Rais Emmanuel Macron katika kampeni yake ya uchaguzi mwaka uliopita, na baraza lake la mawaziri linautaja kuwa muhimu katika juhudi za kuepusha kusambaratika kwa mfumo wa malipo ya uzeeni mnamo miaka ijayo.