Mfalme Charles III wa Uingereza avikwa taji
6 Mei 2023Sherehe ya kumtawaza Mfalme Charles ilisindikizwa na milio ya tarumbeta na imefanyika mbele ya zaidi ya wageni 2,000 wakiwemo viongozi mbalimbali wa dunia na watu maarufu. Askofu mkuu wa Canterbury Justin Welby ndiye aliyemvalisha Mfalme huyo wa Uingereza taji ya dhahabu ikiwa ni ishara ya mamlaka ya utawala wa kifalme katika ibada hiyo ambako Mfalme na mkewe Camilla wameshiriki pia meza takatifu ya Bwana.
Soma zaidi:Maalfu wahudhuria sherehe ya kuvikwa taji mfalme wa Uingereza Charles wa 3
Nje ya kanisa la Wesminster Abbey alikotawazwa Mfalme huyo kulikuwa na askari wa ulinzi elfu kumi pamoja na watazamaji elfu kumi. Wageni waliohudhuria kwenye sherehe hiyo ni pamoja na mke wa Rais wa Marekani Jill Biden, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron,Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau, mawaziri wakuu wanane wa zamani wa Uingereza pamoja na waziri mkuu wa sasa Rishi Sunak. Ujerumani imewakilishwa na rais wake Frank-Walter Steinmeier.
Maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali ya Uingereza na kote duniani waliweka kambi katika njia yenye kilomita mbili ambayo Mfalme Charles III na mkewe Camilla walipita kuelekea kanisa la Westminster Abbey
Kundi dogo la waandamanaji walijikusanya kufuata njia iliyotumiwa na mfalme katika safari yake kutoka katika kasri la Buckingham akiwa kwenye gari lililokokotwa na farasi. Kwa familia ya kifalme na serikali, tukio la kuvikwa taji kwa Mfalme Charles III ni njia ya kuonesha urithi na utamaduni duniani kote.
Mke wa Charles Camilla pia amevishwa taji la umalkia kwenye sherehe ya leo. Shughuli hiyo ilitarajiwa kutazamwa na mamilioni ya watu.
Hata hivyo mwamko na heshima ya tukio hilo vimeonekana kupungua kwa kiasi kikubwa huku watu wengine wakionekana kuto kujali.
Wapinga utawala wa kifalme
Waandamanaji wa vuguvugu la kisiasa la Republican wanaopinga utawala wa kifalme walikusanyika nje na walisikika wakisema "Siyo Mfalme wangu" . Wanadai kuwa taasisi ya kifalme inawakilisha watu wenye uwezo na ukosefu wa usawa katika taifa linaloendelea kuota mizizi ya umasikini na mgawanyiko wa mahusiano ya kijamii.
Soma zaidi:Charles III atangazwa rasmi kuwa Mfalme wa Uingereza
Viongozi wa kundi hilo walikamatwa mapema leo hatua ambayo shirika la kutetea haki za binadamu la Huma Rights Watch imeilaani na kueleza kuwa kitendo hicho kingetarajiwa kushuhudiwa Urusi na siyo Uingereza.
Licha ya waandaaji wa shughuli ya kumvika taji mfalme kusema kuwa hiyo ni ibada takatifu ya kanisa la Anglikana, kwa mara ya kwanza imehusisha ushiriki wa imani nyingine ikiwemo wawakilishi wa dini za Buddha, Waislamu, Wahindu, Wayahudi na dini ya Sikh.