Merkel akutana na wenzake Brussels kuijadili euro
5 Oktoba 2011Safari nyengine ya Kansela Merkel. Mazungumzo mengine na wakubwa wenzake. Dhamira ni moja: kuizamua kanda ya euro inayozama kwenye dimbwi la madeni.
"Tunapoiambia nchi fulani, fanya hivi au fanya vile, punguza nusu ya deni lako, ni nambari nzuri kuzisema. Lakini hicho kinachokuja baadaye ni kile kile. Nalo ni ukweli kwamba hakuna hapa Ulaya anayeweza kununua deni la taifa, maana mtu huwekeza kwenye nchi ambayo kile anachokipata ni kikubwa kuliko kile anachokiingiza." Amesema Kansela Merkel.
Mazungumzo haya ya Brussels yanakuja siku mbili tu, baada ya mengine baina ya mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya huko Luxemborg kushindwa kufikia makubaliano ya kuipatia Ugiriki sehemu iliyobakia ya msaada wa euro bilioni nane, kuiepusha nchi hiyo kufilisika ndani ya wiki chache zijazo.
Badala yake, mawaziri hao waliitaka Ugiriki kuendelea kujitolea muhanga zaidi na kuonya kuwa mabenki huenda yakabeba mzigo mkubwa zaidi wa hasara.
"Sitaki niigize kwamba mwisho wa siku tutakuwa na suluhisho la mgogoro wa kanda ya euro, kinyume na hali halisi ilivyo. Lakini naamini tumepiga hatua fulani mbele. Tunapaswa kuuzingatia uhalisi ulivyo." Amesema Waziri wa Fedha wa Uingereza, George Osborne.
Katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens, wafanyakazi wa sekta ya umma wameupoozesha mji huo kwa mgomo wa masaa 24, wakipinga mpango wa serikali wa kupunguza kazi wafanyakazi 30,000 ili kujiokoa na kuporomoka kabisa kifedha.
Mkurugenzi wa IMF barani Ulaya, Antonio, yupo pia mjini Brussels katika mkutano wa leo na Kansela Merkel, ambapo pia anatarajiwa kutoa muelekeo wa kiuchumi wa kanda ya euro. Tayari IMF imeshasema, kwamba uwezekano wa mtikisiko wa kiuchumi wa ulimwengu hapo mwakani, hauwezi kupuuziwa.
Hofu ya kuibuka kwa mtikisiko imesababisha masoko kuporomoka, ingawa ahadi ya hapo jana ya Kamisheni ya Ulaya ya kuwekeza kwenye mabenki imeziinua hisa kidogo nchini Marekani.
Hata hivyo, barani Asia, bei za hisa zimeendelea kushuka baada ya wafanyabiashara kutilia shaka mpango wa Ubelgiji na Ufaransa kuiokoa benki inayomilikiwa kwa pamoja ya Dexia.
Hapo jana, hisa za benki hiyo zilishuka kwa asilimia 37 kabla ya Ufaransa na Ubelgiji kuingilia kati. Benki hiyo, ambayo inashikilia mabilioni ya deni la Ugiriki na Italia, ilikuwa miongoni mwa benki za mwanzo kulazimika kuingia kwenye mpango wa kufunga mkaja mwaka 2008.
Wasiwasi wa namna mabenki ya Ulaya yatakavyoporomoka ilionekana kukuwa hapo jana, baada ya Waziri Mkuu wa Luxembourg, Jean-Claude Juncker, kuyaonya mabenki hayo kuwa yatarajie hasara ya zaidi asilimia 21 kutoka deni la Ugiriki.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Shäuble, amethibitisha kauli ya Juncker, akiongeza kwamba washikiliaji wote wa dhamana wanaweza kujikuta wakiwa katika hali ngumu sana.
"Wasiwasi mkubwa ni kwamba, katika hali kama hii ya mporomoko katika soko la fedha, basi mgogoro wa kibenki unaweza kuendelea kwa muda mrefu." Amesema Waziri Shäuble.
Mabenki mengi ya Ulaya, hasa hasa ya nchini Ufaransa, yanashikilia kiwango kikubwa cha dhamana ya deni la nje la Ugiriki, na ili ziweze kuhimili mtikisiko huu wa sasa, ni lazima zisaidiwe na serikali zao.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Josephat Charo