1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo Ugiriki kupinga hatua zaidi za kubana matumizi

5 Oktoba 2011
https://p.dw.com/p/Rp9x
Mgomo wasababisha usumbufu kwa abiria katika uwanja wa ndege wa Athens .Picha: AP

Shughuli za umma nchini Ugiriki zimezorota kabisa leo kutokana na mgomo kote nchini ambao pia umevuruga usafiri wa ndege. Wafanya kazi wa serikali nchini humo wanaupinga mpango wa kubana matumizi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na mzigo mkubwa wa madeni ya nchi hiyo.

Mgomo huo wa saa 24, umezorotesha shughuli zote za usafiri wa reli, huku shule na mahakama zikifungwa , wakati hospitali zimelazimika kuwaita wafanyakazi wa dharura. Maeneo ya utalii kama makumbusho na sehemu za kale za kihistoria pia yamefungwa.

Wafanyakazi wa serikali wanaupinga mpango wa kuwapunguzia mishahara waajiriwa kiasi ya 30,000 ambao tayari mishahara ilipunguzwa mwaka uliopita.

Mgomo huo unaungwa mkono na chama kikuu cha wafanyakazi nchini Ugiriki, ambacho kimeitisha mgomo mkuu kupinga hatua za serikali tarehe 19 mwezi huu.

Wakati serikali ikijaribu kutafuta njia za kupunguza mzigo wake wa madeni, mpango wake umezusha malalamiko hata ndani ya chama tawala chenyewe cha Kisoshalisti.

Mipango ya kubana matumizi ni sharti kuu lililotolewa kwa Ugiriki na wakopeshaji wa kimataifa-Shirika la fedha la kimataifa IMF na Benki kuu ya Ulaya-kufuatana na mpango wa kufufua uchumi ulioanzishwa mwaka jana, ili nchi hiyo iweze kupatiwa mkopo wa euro 149 bilioni.

Wachambuzi wanasema chama tawala cha Kisoshalisti ambacho kiko nyuma ya kile cha kihafidhina cha Conservative, katika uchunguzi wa kura za maoni, hakina chaguo jengine isipokuwa kutekeleza marekebisho yaliopendekezwa na Shirika la fedha la kimataifa na Umoja wa Ulaya , licha ya upinzani mkubwa nyumbani.

Kwa wakati huu ujumbe wa ngazi ya juu kutoka taasisi hizo mbili za fedha pamoja na umoja wa ulaya uko nchini Ugiriki ukichunguza mahesabu ya fedha, wakati Hazina ya serikali ya Ugiriki kuweza kulipa mishahara ya wafanyakazi na malipo ya uzeeni inamalizika mwezi ujao wa Novemba.

Matokeo ya uchunguzi wao ndiyo yatakayoamua iwapo taasisi hizo tatu ziipe Ugiriki mkopo wa euro bilioni nane mwezi ujao au la.

Wakati huo huo hisa katika soko la fedha mjini Athens leo zimeanguka katika kiwango kisichowahi kuonekana kwa miaka 18, baada ya maafisa wa Umoja wa Ulaya kuahirisha hatua ya kuikwamua Ugiriki .

Umoja huo uliahirisha kutoa fedha hizo, ukiitaka Ugiriki ichukuwe hatua zaidi ukionya kwamba mabenki yatapaswa kubeba mzigo wa hasara zaidi, ikiwa ni sehemu ya azimio la kukabiliana na msukosuko wa madeni.

Katika kujaribu kuituliza hali ya mambo na kuondoa wasi wasi uliopo miongoni mwa jamii, waziri wa fedha wa Ugiriki alisema hapo jana kwamba hapahitajiki hatua zaidi za kubana matumizi.

Mbali na mgomo huo mkuu kunafanyika pia maandamano katika miji mikubwa ya Athens na Thessaloniki.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/afp

Mhariri:Josephat Charo