1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kuunda serikali ya muunano waendelea Italia

Amina Abubakar Daniel Gakuba
22 Agosti 2019

Kiongozi wa chama cha Democratic nchini Italia Nicola Zingaretti ameonya chama hicho hakiko tayari kuunda serikali ya muungano na chama hasimu cha vuguvugu la nyota tano M5S.

https://p.dw.com/p/3OL2r
Regierungskrise in Italien | Matteo Salvini
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Serikali ya muungano kati ya vyama hivyo viwili chama cha Democratic chenye sera za mrengo wa kushoto nchini humo na chama cha vuguvugu la nyota tano M5S ndio njia pekee ya kuzuwia uchaguzi wa mapema, ambao iwapo utafanyika basi kiongozi wa chama cha Ligi kinachopinga wahamiaji Matteo Salvini huenda akashinda uchaguzi huo.

Lakini baada ya kuwa na mazungumzo na rais wa Italia Sergio Mattarella, kiongozi wa chama cha Democratic Nicola Zingaretti amesema haitokuwa rahisi kwa chama chake kufanya kazi na watu wanaotofautiana kisiasa.

Italien Rom Regierungsbildung
Rais wa Italia Sergio MattarellaPicha: Imago/IPA/M. Trex

"Sio chaguo rahisi kwetu kwa sababu ya mzigo ambao serikali iliyokuwepo imetuachia, na kwasababu tuna mtazamo tofauti wa kisiasa  na watu wengine hasa chama cha vuguvugu la nyota tano, washirika wa serikali ya Conte. Lakini tuna wasiwasi kuhusu changamoto iliopo katika uchumi wetu," alisema Zingaretti.

Nicola Zingaretti amesema iwapo serikali hiyo itaundwa na vyama hivyo viwili basi ni lazima kwanza chama cha M5S kikubali kufuata sera za kuiunga mkono Umoja wa Ulaya na kuunga mkono suala la uhuru wa wahamiaji.

Kiongozi wa chama cha M5S adaiwa kutoa maagizo yasio kuwa na msingi

Hata hivyo Manlio Di Stefano, Waziri Mdogo wa mambo ya kigeni anaeondoka anayetokea chana cha vuguvugu la nyota tano M5S amekanusha matamshi ya Zingareti akisema kiongozi huyo anacheza mchezo wa kujifanya hataki kinachopendekezwa huku akitoa matakwa ambayo hayana msingi.

Vorwahlen PD Italien | Neuer Vorsitzender Nicola Zingaretti
Kiongozi wa chama cha Democratic nchini Italia Nicola ZingarettiPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/C. Fabiano

Italia imeingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Waziri wa mambo ya ndani Matteo Salvini kuitisha kura ya kutokuwa na imani na serikali ya muungano iliyodumu miezi 14 kati ya chama chake na chama cha M5S akitumai uchaguzi wa mapema utafanyika na kutarajia kuchukua ushindi. Hatua yake hiyo ilimlazimisha waziri mkuu Giuseppe Conte kujiuzulu.

Rais  Sergio Mattarella amekuwa akikutana na viongozi wa kisiasa nchini humo kuona iwapo kuna nafasi ya kuunda muungano mbadala wa utawala au iwapo uchaguzi wa mapema ufanyike ikiwezekana mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Mattarella anatarajiwa kukutana na Matteo Salvini pamoja na kiongozi wa chama cha M5S Luigi Di Maio.

Vyanzo:dpa/reuters