Mazingira yasababisha aina mpya ya wakimbizi
16 Novemba 2005Wakimbizi wa mazingira ni aina mpya ya wakimbizi ambao hawawezi tena kupata riziki yao ya kila siku kwa sababu ya ukame, mmomonyoko wa udongo, kuenea kwa jangwa, uharibifu wa misitu na matatizo mengine ya kimazingira. Katika hali yao ya kutapatapa kwa sababu ya ongezeko kubwa la idadi ya wakaazi na umaskini, watu hawa huhisi hawana chaguo lengine ila kutafuta ufadhili katika maeneo mengine ya dunia, bila kujali hatari inayoweza kuwapata.
Wengi wamelazimika kuyahama makazi yao kwenda kuishi sehemu nyengine ya taifa lao, lakini sio wote waliozikimbia nchi zao. Lililo wazi ni kwamba wahamiaji wa mazingira wameyahama maskani yao aidha kwa mda au kabisa, huku wakiwa na matumaini machache ya kurudi kwao.
Inakadiriwa kuna takriban wakimbizi wa mazingira milioni 25 ikilinganishwa na wakimbizi wa kawaida milioni 27. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka mara mbili kufikia mwaka wa 2010. Kufuatia kuongezeka kwa uoto duniani, inakadiriwa watu milioni 200 watapoteza makao kwa sababu ya vimbunga, ukame wa mda mrefu na mafuriko kwenye pwani za bahari yatakayosababishwa na ongezeko la kiwango cha maji baharini.
Akizungumza katika warsha iliyoandaliwa na wakfu wa Konrad Adenauer Stiftung katika eneo la Wesseling hapa Bonn, profesa Wolfgang Gieler, wa chuo kikuu cha Okan mjini Istanbul, alisema Afrika imeathiriwa sana huku raia milioni 8 wa Sudan, milioni 6 wa Somalia na wakenya milioni 3 wakikabiliwa na njaa. Alisema pia kwamba China ina wakimbizi wa mazingira takriban milioni 6 ambao wameyahama makazi yao kwa ukosefu wa mashamba ya kulima. Miradi mikubwa ya serikali kama vile ujenzi wa barabara au mabwawa ya maji imelaumiwa kama njia mojawapo inayosababisha wakimbizi wa mazingira.
Watu takriban bilioni moja walioongezeka duniani katika miaka ya 1990, wengi wanaishi chini ya kiwango cha dola moja ya kimarekani. Wengi wanatakiwa kuwa wakulima wadogo wanaojitahidi kupata riziki ya kuendelea kuishi katika mazingira yaliyofunikwa na maji yaliyokauka sana au yaliyo na milima kiasi cha kutoweza kulimika. Umaskini huzidisha matatizo ya kimazingira ambayo huwalazimu watu kuhama, pamoja na idadi kubwa ya wakaazi, unyanyapaa, ukosefu wa ardhi, ukosefu wa ajira, kukua haraka kwa miji, magonjwa ya kuambukizwa, sera mbaya za serikali na machafuko ya mara kwa mara.
Ni vigumu kutofautisha kati ya wakimbizi wa mazingira na wale wa wanaohama kwa sababu za kiuchumi. Tatizo lengine ni kutotambuliwa rasmi na serikali na mashirika ya kimataifa kwamba kuna shida ya wakimbizi wa mazingira. Wakimbizi hawa wanatishia kuzusha mzozo mkubwa wa kibinadamu katika muongo huu.
Wakimbizi wengi hukimbilia katika mataifa yaliyoendelea hususan barani Ulaya. Wanapofika hutumiwa kufanya kazi kwa maplipo kidogo ikilinganishwa na raia wa mataifa wanakofikia. Ni kwa umbali gani mataifa yaliyoendelea yameweza kuwatumia wakimbizi kujinufaisha kiuchumi? Bwana Wolfgang anafikiri swala hili linaweza kuangaliwa kwa mtazamo mwingine, kwa sababu kuna hitaji la wafanyikazi walio rahisi kuwalipa katika mataifa yaliyoendelea kiviwanda dunaini. Mataifa haya yanatumia nafasi hii kupunguza gharama za kiuchumi.
Ili kukabiliana na tatizo la wakimbizi wa mazingira ipo haja ya kuwashughulikia kama wakimbizi wengine. Haiwezekani kuwapuuza eti kwa sababu hakuna taasisi maalumu zinazoyajali maslahi yao. Kuna haja kubwa ya kuelewa shina la tatizo hili, sio tu mazingira bali pia usalama. Lakini kutakuwa na ufanisi mdogo pasipo kudhamini maendeleo endelevu katika maeneo yaliyoathiriwa kama vile pembe ya Afrika, Asia ya kati na katika milima ya Himalaya na Caucasus.