1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauti ya Osama utata kama ulivyokuwa uhai wake

5 Mei 2011

Licha ya wanasiasa Marekani kuinyooshea kidole Pakistan kwa madai ya kukumbatia ugaidi, Umoja wa Ulaya umejitokeza kuiunga mkono nchi hiyo na kutaka isaidiwe na sio kulaumiwa.

https://p.dw.com/p/119ei
Osama bin Laden wakati wa uhai wake
Osama bin Laden wakati wa uhai wakePicha: AP

Msemaji wa Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema hivi leo mjini Brussels, kwamba hiki ni kipindi ambacho Pakistan inahitaji zaidi msaada wa kupambana na ugaidi na kuimarisha demokrasia, kuliko wakati mwengine wowote huko nyuma.

Msemaji huyo, Michael Mann, amesema kwamba ulimwengu utaendelea kuitegemea Pakistan katika vita vyake dhidi ya ugaidi na, kwa hivyo, ni lazima kuisaidia serikali ya waziri mkuu Yusuf Raza Ghilani, kufanikisha vita hivi.

Mann ameonya kuwa kifo cha kiongozi wa Al-Qaida kinapaswa kutoa funzo la kuoanisha mapambano dhidi ya ugaidi na haki za binaadamu. Bila ya kutaja namna kifo cha Bin Laden kilivyotokea, kauli hii ya Umoja wa Ulaya inapingana na mawazo ya jumla ya wanasiasa wa Marekani kuhusiana na kifo hicho na dhima binafsi ya Pakistan.

Nyumba inayoaminika kuwa kiongozi wa Al-Qaida, Osama bin Laden, alikuwa akiishi
Nyumba inayoaminika kuwa kiongozi wa Al-Qaida, Osama bin Laden, alikuwa akiishiPicha: dapd

Waziri wa Mambo wa Nje wa Pakistan, Salman Bashir, amesema kwamba si haki kuilaumu nchi yake kwa sababu tu Bin Laden ameuawa ndani ya ardhi yake, kwani inafahamika namna ilivyojitolea kwenye mapambano haya.

"Ni rahisi kusema kuwa Idara yetu ya Ujasusi au watu fulani kwenye serikali wana uhusiano na Al-Qaida. Hii ni dhana ya uongo. Haiwezi kuthibitishwa katika mazingira yoyote yale na inapingana na kile ambacho Pakistan na hasa Idara ya Ujasusi imekuwa ikifanya." Bashir amewaambia waandishi wa habari mjini Islamadab hivi leo.

Wakati huo huo, Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pilley, ametaka Marekani izichapisha picha za mkasa mzima wa kuuawa kwa Bin Laden. Pilley amesema kwamba, ulimwengu una haki ya kujitosheleza kuwa mauaji haya yalifanyika kwenye misingi ya kisheria.

Akijibu wito huo, Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Eric Holder, ameendelea kutetea msimamo wa serikali yake kumuua Bin Laden, akidai kwamba hata kama kiongozi huyo wa Al-Qaida hakuwa na silaha, hapakuwa na dalili kwamba alikuwa tayari kujisalimisha.

Hata hivyo, madai haya yanapingana na taarifa iliyotangazwa leo na kituo cha televisheni cha Al-Arabiya, ambayo imemnukuu binti wa miaka 12 wa Bin Laden, aliyekuwepo wakati wa mkasa huu, akisema kwamba baba yake aliuawa akiwa chini ya ulinzi wa majeshi ya Marekani.

Rais Barack Obama na timu yake wakifuatilia mkasa wa kuvamiwa na baadaye kuuawa kwa Osama bin Laden
Rais Barack Obama na timu yake wakifuatilia mkasa wa kuvamiwa na baadaye kuuawa kwa Osama bin LadenPicha: The White House, Pete Souza/AP

Hatima ya Bin Laden mikononi mwa majeshi ya Marekani sasa imekuwa ndio mada kubwa kuliko hata ukweli wa ama kutokea au kutotokea kwa kifo chake.

Mapema leo kiongozi wa kanisa la Kianglikana duniani, Askofu Mkuu wa Canterbury, Rowan Williams, alieleza kutokuridhika kwake na namna mauaji haya yalivyotokea.

"Nafikiria kuwa mauaji ya mtu asiyekuwa na silaha yataendelea kuwa jambo lisiloridhisha, maana inaelekea kama kwamba haki haikuonekana ikitendeka." Amesema Askofu Mkuu Williams.

Nchini Pakistan kwenyewe, ambako mauaji hayo yalifanyika, serikali imeonya hatari ya mashambulizi ya kigaidi kulipiza kisasi, huku chama kikuu cha upinzani, Jamaat-e-Islam, kikiitisha maandamano baada ya sala ya Ijumaa ya kesho, kushinikiza serikali ijitoe kwenye usuhuba na Marekani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi