1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taarifa zaidi kuhusu kifo cha Osama zajitokeza

4 Mei 2011

Kilichomtokezea Osama bin Laden mwisho wa masiha yake, sasa kinazidi kuibuka na utawala wa Rais Barack Obama unakiri kwamba kiongozi huyo wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaida hakuwa amejihami kwa silaha.

https://p.dw.com/p/118ew
Osama bin Laden wakati wa uhai wake
Osama bin Laden wakati wa uhai wakePicha: AP

Ni kama kwamba Osama Bin Laden amekataa kufa hata baada ya kuuawa na majeshi ya Marekani. Taarifa kuhusu namna mauti yalivyomkumba, sasa zimekuwa muhimu zaidi kuliko mauti yenyewe, na sasa maswali yamekuwa ni vipi na kwa nini aliuawa, na sio ukweli ama uongo wa kifo chake.

Jioni ya jana, Ikulu ya Marekani ilitoa taarifa mpya juu ya namna kifo hicho kilivyotokezea, ambayo kwa kiasi kikubwa inatafautiana na ile iliyotolewa juzi na Rais Obama, wakati akiutangazia ulimwengu kifo hicho cha Bin Laden.

Katika taarifa hii mpya, msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jan Carney, amesema kwamba Bin Laden alikutwa chumbani akiwa na mke wake, hakuwa na silaha, na kwamba aliyeonesha purukushani kidogo ni mke wake, ambaye hatimaye alipigwa risasi ya mguu. Ni hapo ndipo Bin Laden alipopigwa risasi na kuuawa, kwa mujibu wa Carney.

Katika tangazo la kifo cha Bin Laden hapo juzi usiku, Rais Obama, ambaye baadaye ilifahamika kwamba alikesha kufuatilia mkasa mzima ulivyokwenda huko Abbotabbad, Pakistan, alisema kwamba Osama alikuwa amejihami kwa silaha na kwamba aliuawa wakati wa makabiliano na baadaye mwili wake kuchukuliwa na wanajeshi wa Marekani.

Taarifa za Ikulu ya Marekani zakosolewa

Rais Barack Obama akitangaza kifo cha Osama bin Laden hapo juzi
Rais Barack Obama akitangaza kifo cha Osama bin Laden hapo juziPicha: AP

Hata hivyo, mara tu baada ya kutolewa kwa taarifa hii mpya ya Ikulu ya Marekani, makundi mbali mbali ya haki za binaadamu, waandishi na wachambuzi wa masuala ya usalama, wamejitokeza ama kuzihoji taarifa zote mbili au kuzipinga na kutaka uwazi zaidi juu ya mkasa mzima ulivyotokezea.

Kansela wa zamani wa iliyokuwa Ujerumani ya Magharibi, Helmut Schmidt, amekiambia kituo kimoja cha televisheni hapa Ujerumani, kwamba kwa ujumla operesheni hii itakuwa na athari kubwa kwa ulimwengu wa Kiarabu, ambako kwenyewe hivi sasa kunakabiliwa na wimbi la mapinduzi ya umma, na kuiita operesheni hii kuwa ni "uvunjwaji wa wazi wa sheria za kimataifa".

Naye mwanasheria na mwanaharakati mkubwa wa haki za binaadamu nchini Australia, Geoffrey Robertson, amenukuliwa na Shirika la Habari la Australia (ABC), akisema kwamba, haki haikutendeka.

"Si sheria hata kidogo. Sheria inamaanisha kumpeleka mtu mahakamani. ambako baada ya kumkuta na hatia anahukumiwa. Kilichompata Osama ni adhabu ya kunyongwa haraka haraka. Kinachoonekana kupitia upotoshaji mkubwa wa habari unaofanywa na Ikulu ya Marekani, ni kwamba haya yalikuwa mauaji tu." Amesema Robertson.

Watu kadhaa wamekuwa wakiitaka Ikulu ya Marekani ichapishe hadharani picha za mkasa mzima wa tukio hili la mauaji ya Bin Laden. Hadi sasa, jambo hili linapingwa na Ikulu hiyo kwa madai kwamba, linaweza kuchochea hamasa na kisasi kutoka kwa wafuasi wa kiongozi huyo ya Al-Qaeda, japokuwa inashikilia kutaka kuaminiwa na ulimwengu.

"Tufanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hakuna mwenye hoja ya kujaribu kukanusha kwamba tuliyemuua ni Osama bin Laden. Na kwa hivyo, utowaji wa taarifa, hata kama utahusisha picha zenyewe, linabakia suala la kujadiliwa na kuamuliwa." Alisema John Brennan, mshauri wa Rais Obama katika masuala ya vita dhidi ya ugaidi.

Kwa mujibu wa mwanasheria Robertson, kwa kumuua Bin Laden, Marekani imempa kiongozi huyo wa Al-Qaida kile hasa ambacho alikuwa akikitaka, nacho ni kufa kwa risasi akiwa kwenye uwanja wa mapambano, badala ya kumalizia maisha yake jela au kwenye kitanzi.

Na hili linamfanya kuonekana zaidi shujaa na shahidi mbele ya wafuasi wake, kuliko gaidi na mhalifu, kama ambavyo ameaminika kuwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman